TAHARIRI: Idadi ya watu isizidi maendeleo ya nchi
Na MHARIRI
KILA mara ripoti kuhusu takwimu za watu nchini zinapotolewa, suala linaloibuka miongoni mwa wananchi wengi ni kuhusu siasa.
Utakuta midahalo inayosheheni mitandao ya kijamii na maeneo mengine ambapo watu hujumuika ni kuhusu makabila yaliyo na idadi kubwa ya watu, yale yaliyo na upungufu wa watu na jinsi idadi hizo zitakavyotumiwa kisiasa uchaguzini.
Si vibaya kutabiri mkondo wa kisiasa kwa kutumia takwimu hizi, lakini inafaa mambo yanayohusu maendeleo yapewe uzito zaidi.
Ni nadra sana kupata watu wakijadiliana kuhusu jinsi takwimu za idadi ya watu zinavyoweza kutumiwa kutabiri mkondo wa maendeleo na uchumi wa nchi.
Hata wakati baadhi ya vyombo vya habari vitakapojizatiti kufanya uchanganuzi wa kina katika kulinganisha idadi ya watu na maendeleo, ni wananchi wachache sana ambao watatilia maanani masuala hayo.
Hivi sasa, kuna wengi wanaosherehekea jinsi idadi ya makabila yao ilivyoongezeka. Hakika, kwa jumla idadi ya watu imeongezeka kitaifa.
Kile tunachofaa kujiuliza ni ikiwa kweli tuna rasilimali za kutosheleza mahitaji ya idadi hii ya watu inayoongezeka.
Hivi sasa, nchi hii inakumbwa na changamoto tele katika uzalishaji wa chakula cha kutosha, utoaji huduma bora za afya kwa bei nafuu, na huduma bora za elimu.
Ilivyobainika kwenye ripoti ya Idara ya Takwimu za Kitaifa (KNBS), hata hali ya makao ni mbovu mno kwa mamilioni ya Wakenya.
Imebainika, ni wananchi wachache sana wanaoishi katika nyumba nadhifu, huku mamilioni wakitegemea nyumba zilizojengwa kwa nyasi na udongo.
Tunaweza kulaumu wanasiasa kwa kufanya raia waamini kuwa ni muhimu kuzaana kwa wingi, eti kwa vile hiyo ni njia ya kuongeza kura za jamii na kupeleka mmoja wao hadi Ikulu.
Wanasiasa wetu wengi ni wabinafsi, na kamwe hawajali kuhusu mahitaji ya umma.
Wametelekeza majukumu yao ya kuhudumia wananchi vyema ilhali wangali wanapigia debe watu wazaane kwa wingi.
Kuna mataifa ambayo kweli yameimarika kwa kutumia idadi yao kubwa ya watu kujiletea maendeleo, lakini tujiulize, je, Kenya imefikia uwezo wa kuhitaji idadi kubwa ya watu kuendesha uchumi wake au ongezeko hili litakuwa ni laana?