Habari Mseto

Hoja ya kuzima uuzaji muguka yaibua maoni mseto

February 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

WATAFUNAJI muguka Kaunti ya Lamu watalazimika kusafiri hadi nje ya eneo hilo ili kutafuta bidhaa hiyo, endapo hoja ya kupiga marufuku uraibu huo itapitishwa na Bunge la Kaunti ya Lamu wiki hii.

Diwani wa Wadi ya Mkunumbi, Bw Paul Kimani Njuguna, ambaye pia ni Naibu Spika katika Bunge la Lamu, alisema anapanga kuwasilisha hoja bungeni katikati ya wiki inayopendekeza marufuku kwa usambazaji, uuzaji na ulaji muguka kote Lamu.

Kulingana na Bw Njuguna, bidhaa hiyo imesababisha maisha ya vijana wengi Lamu kuharibika kwa kuwa wamejitosa katika uraibu huo na kukosa kuwajibikia masuala ya ujenzi wa taifa na maendeleo.

Bw Njuguna pia alilaumu desturi ya utafunaji muguka kwa kuchangia idadi kubwa ya wanafunzi wanaoacha shule na kupotelea katika uraibu huo.

Alisema ni kupitia marufuku ya muguka ambapo pia talaka nyingi zinazoshuhudiwa Lamu kila kuchao zitapungua.

Alisema familia nyingi zimezongwa na umaskini kutokana na kwamba wanaostahili kuziinua wamepotelea katika utafunaji wa muguka.

Alisema anaamini madiwani wenzake katika bunge hilo watamuunga mkono kwa kauli moja ili kuona kwamba muguka unapigwa marufuku Lamu ili kuokoa kizazi cha siku zijazo.

“Nimejiandaa kuwasilisha hoja Bungeni Lamu juma hili. Hoja hiyo inapendekeza muguka kupigwa marufuku, ambapo hautaruhusiwa kuingizwa, kuuzwa au kutafunwa eneo hili. Haya yote ni kutokana na athari mbaya ambazo umeleta kwa jamii yetu,” alisema

Akaongeza, “Vijana, wakiwemo wanafunzi wa shule wamepotelea katika utafunaji wa muguka kutokana na kwamba ni rahisi kuupata. Isitoshe, wanaume na hata akina mama hawawajibikii vilivyo familia zao. Kila pesa wanazopata wako mbioni kununua muguka. Umaskini umekithiri miongoni mwa familia nyingi hapa Lamu kwa sababu ya muguka,” akasema Bw Njuguna.

Baadhi ya wafanyabiashara wa miraa na muguka, Kaunti ya Lamu aidha wamepinga vikali mpango wa huo wakidai ni njama ya kuwaharibia biashara yao.

Mwenyekiti wa Jamii ya Wameru, Kaunti ya Lamu, Bw Jacob Muroki, alisema hoja hiyo pia inalenga jamii husika ya Wameru ambao ndio waliojikita katika biashara ya miraa na muguka.

Alipinga madai kwamba miraa inauziwa watoto wadogo, akisisitiza kuwa ipo haja ya wazazi wenyewe kuwajibikia malezi ya watoto wao badala ya kuwanyoshea wafanyabiashara kidole cha lawama.

“Kwanza miraa na muguka inakubalika kikatiba. Inakuaje leo hili bunge la Lamu linataka kupiga marufuku ulaji muguka. Hiyo ni njama ya kufungia nje jamii ya Wameru ambao wamejikita sana katika biashara ya muguka,” akasema Bw Muroki.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw John Kirea ambaye ni muuzaji mashuhuri wa muguka mjini Lamu aliyesisitiza kuwa muguka huuziwa watu wazima pekee na wala si watoto.

Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Miraa, Kaunti ya Lamu, Bw Ibrahim Kamanja, alilitaka bunge la kaunti ya Lamu kujadili hoja zinazoleta manufaa kwa wananchi na hata kuwajenga badala ya kuwabomoa.