• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Red Cross yawafadhili Waboni kwa biashara na kilimo

Red Cross yawafadhili Waboni kwa biashara na kilimo

NA KALUME KAZUNGU

SHIRIKA la Msalaba Mwekundu limezindua mpango maalum unaolenga kuisaidia jamii ya Waboni katika kaunti ya Lamu kubadili maisha kwa kuwafadhili kibiashara, kilimo na uvuvi.

Tangu jadi, wakazi wa jamii ya Waboni wamekuwa wakitegemea maisha ya msituni, ambapo shughuli zao ni kuwinda wanyama pori, kuvuna asali pamoja na kuchuma matunda ya mwituni.

Aidha tangu 2015 baada ya serikali ya kitaifa kuzindua operesheni ya Linda Boni inayolenga kuwafurusha au kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab ndani ya msitu wa Boni, jamii hiyo haijaruhusiwa kuendeleza shughuli kama kawaida kutokana na sababu za kiusalama.

Akizungumza na Taifa Leo ofisini mwake Jumatano, Mshirikishi Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Lamu, Bi Kauthar Alwy, alisema tayari wamelenga zaidi ya familia 1000 kutoka vijijiji vyote vya Waboni ili kuzifadhili kibiashara, ukulima na uvuvi.

Vijiji vinavyolenga ni Basuba, Milimani, Mararani, Mangai, Kiangwe, Bodhei, Pandanguo,  Ndununi, Ingini, Ishakani, Madina na Bar’goni.

Kulingana na Bi Kauthar, mradi huo unalenga hasa kuwawezesha Waboni kuacha maisha ya kuwinda wanyama, kutafuta asali na kuchuma matunda ya mwituni na badala yake kugeukia maisha ya kisasa, ikiwemo kilimo, biashara na uvuvi.

“Waboni wamekuwa wakiteseka hasa tangu kuzinduliwa kwa operesheni inayoendelea ya Linda Boni. Hawawezi kutegemea msitu wao tena ili kuendeleza uvunaji asali, uwindaji wanyama pori au matunda ya mwituni kama desturi yao.

Hii ndiyo sababu Shirika la Msalaba Mwekundu likaibuka na mpango huo wa kuwafadhili Waboni kwa uvuvi, kilimo na biashara. Lengo letu ni kuiwezesha jamii ya Waboni kujikimu maishani badala ya kutegemea misaada ya serikali. Mradi pia unalenga kuinua maisha ya Waboni kwa jumla,” akasema Bi Kauthar.

Ufadhili wa kilimo unatekelezwa kwenye vijiji vya Basuba, Milimani, Mararani, Mangai, Kiangwe, Bodhei na Pandanguo ilhali ule wa biashara unatekelezwa kwa Waboni wanaoishi kijijini Bar’goni.

Shirika hilo pia limetoa vifaa vya uvuvi kwa Waboni wanaoishi vijiji vinavyopakana na Bahari Hindi, ikiwemo Ishakani, Kiangwe, Ndununi, Ingini na Madina.

Mradi huo aidha umepongezwa na wakazi wa jamii ya Waboni ambao hawakuficha furaha yao kufuatia ufadhili huo.

Mzee wa kijiji cha Pandanguo, Bw Aden Golja, alisema wamepokea chakula, mbegu na pembejeo kutoka kwa shirika hilo na tayari wameanza shughuli za upanzi.

“Tumefurahia ufadhili huo na kila mmoja wetu tayari anaendelea kujituma mashambani. Pia tumepokea msaada wa chakula kitakachotusaidia kuendeleza kilimo eneo letu,” akasema Bw Golja.

You can share this post!

Kituo maalum cha watalii chazinduliwa Lamu

Wenye ardhi wataka wafidiwe

adminleo