Wafanyakazi wachafua jiji wakidai malipo ya miezi 3
SAMMY KIMATU na CECIL ODONGO
WAKAZI katika Kaunti ya Nairobi walipigwa na butwaa kufika katikati mwa jiji na kukuta jiji limegeuzwa kuwa jaa la taka Jumanne asubuhi.
Wengi wa waliokumbana na takataka hizo ni wale wanaorauka mapema asubuhi kwenda kununua bidhaa kutoka Soko la Gikomba, Muthurwa na pia soko la Wakulima linalofahamika na wengi kama Marikiti.
Waziri wa Mazingira wa Kaunti ya Nairobi, Bw Larry Wambua alikiri kwamba wazoaji taka hao hawajalipwa mishahara yao kwa miezi mitatu lakini hakufichua ni kiasi gani.
“Nafahamu kwamba mgomo huo umesababishwa na wafanyakazi kukosa kupokea mishahara kwa miezi mitatu. Hata hivyo, jukumu hilo ni la wizara ya fedha ambayo bado halina msimamizi,” akasema Bw Wambua.
Afisa Mkuu wa Mipango ya Kiuchumi wa Nairobi , Bw Washington Makodingo naye alilaumu idara ya mazingira, akisema haikuwasilisha orodha ya majina ya wanakandarasi wazoaji taka ili walipwe kwa wakati.
“Idara ya mazingira haifai kutulaumu kwa sababu wao ndio walikosa kutimiza wajibu wao,” akasema Bw Makodingo.
Asubuhi, wahudumu wa teksi na pia waendeshaji matatu walishuhudia kilichokuwa kikiendelea kati ya saa sita hadi za kumi asubuhi, ambapo taka hizo zilikuwa zikimwagwa.
Mfanyabiashara katika soko la Muthurwa ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema malori ya kusafirisha taka yalitumika kueneza uchafu huo. Mama huyo anayeuza nyanya katika soko hilo, alisema kuwa malori hayo yalikuwa yakibeba takataka na kuzimwaga karibu na sehemu wanapouzia bidhaa zao.
“Kazi ya kuleta taka hapa ilikuwa ya malori yaliyopewa kandarasi na serikali ya Gavana Mike Sonko. Wanafanya hivyo kwa kukosa kulipwa kwa miezi mitatu,” mama huyo aliambia Taifa Leo.
Maeneo mengine ambapo pia taka zilimwagwa ni kituo cha mabasi cha Machakos, Soko la Retail, nje ya Soko la wakulima na mzunguko wa Haile selassie na barabara ya Landhies.
Kando na huko, sehemu nyingine za katikati mwa njiji pia zilikumbana na takataka hizo zilizotapakaa katika kituo cha mabas cha Bus Station, barabara ya Mfangano, Ronald Ngala, Kimathi Street, Uhuru Highway na Steji ya GPO.
Kilichowashangaza wengi asubuhi ni sababu ya takataka kusambazwa chini ya mapipa jijini, kabla ya kubaini mzozo unaoendelea.
“Watu hao hawakuwa wakiogopa kamera za CCTV zilizoko katikati mwa jiji wala kuogopa kukamatwa na polisi. Kuna wale tunajua ni wa Sonko wakichanganyikana mahasidi wake ili masaibu yake yaongezeke ndipo aonekane ni mbaya zaidi,” mlinzi katika jumba moja jijini aliambia Taifa Leo.
Wiki jana, Gavana Mike Sonko alitia saini mkataba na waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa wa kupeana wizara nne kuu kutoka kwa kaunti na kuzikabidhi kwa serikali kuu. Mkataba huo ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi na kushuhudiwa na Rais Uhuru Kenyatta.