Habari Mseto

Magavana wapendekeza mfumo mseto na mgao wa asilimia 45

March 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA sasa wamebadili msimamo wao wa awali kuhusu mfumo wa utawala wa ubunge na badala yake kuunga mkono kupanuliwa kwa kitengo cha utawala kwa kubuniwa nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wawili.

Aidha wanataka kaunti zitengewe asilimia 45 ya mapato ya serikali.

Chini ya mwavuli wa baraza lao (CoG) wakuu hao wa kaunti pia wanapendekeza Katiba ifanyiwe mageuzi ili kubuniwe afisi ya Kiongozi wa Upinzani na idadi ya mawaziri iwe 18 pamoja na manaibu 22.

Wakiwasilisha mapendekezo yao kwa Kamati ya Maridhiano (BBI) Ijumaa kupitia mwenyekiti wa baraza hilo Wycliffe Oparanya, hata hivyo wanataka Waziri Mkuu awe kiongozi wa Serikali na Rais awe kiongozi wa taifa.

“Thuluthi moja ya mawaziri wanafaa kuteuliwa nje ya bunge ilhali manaibu 22 wawe wabunge,” Bw Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kakamega, akasema.

Aliongeza kuwa uteuzi wa mawaziri sharti uafiki kanuni ya usawa wa kijinsia na uakisi maeneo yote nchini.

Bw Oparanya alikuwa ameandamana na magavana; Anne Waiguru (Kirinyaga), Wycliffe Wangamati (Bungoma) na James Ongwae (Kisii).

Katika memoranda iliyosomwa kwa Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji, baraza hilo lilikuwa limependekeza mfumo wa utawala wa ubunge likisema ungehakikisha kuwa maeneo yote nchini yanashirikishwa serikalini.

Magavana hao walisema kuwa mfumo huo ungezuia uwezekano wa kutokea kwa ghasia za kisiasa na kuhakikisha kuwa Katiba inaupa nguvu upinzani.

Lakini walipoanza kuichambua memoranda hiyo, magavana hao waliondoa pendekezo hilo bila kutoa sababu zozote.

Vilevile, wanapendekeza Bunge la Seneti liongezwe hadhi ili liwe na mamlaka kuliko Bunge la Kitaifa.

Bw Oparanya na wenzake wanataka Seneti ipewe mamlaka ya kuidhinisha mikataba yote ya kimataifa na miswada yote ikiwemo ile ambaye inahusishwa matumizi ya fedha za umma.

“Vile vile, tunapendekeza kwamba kaunti zote 47 zidumishwe. Na tunapinga miito ya kutaka Kaunti ya Nairobi itwaliwe na Serikali ya Kitaifa,” wakasema katika memoranda yao kwa kamati ya Bw Haji.

Na ili kukomesha mivutano ya kila mara kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB) kati ya Serikali Kuu na zile za Kaunti, magavana hao wanapedekeza kuwa mapendekezo ya Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kuhusu suala hilo ndiyo yazingatiwe.

“Na tunataka mgao kwa serikali za kaunti uwe ni asilimia 45 ya jumla ya mapato ya serikali badala ya asilimia 15 ilivyo sasa,” Bw Oparanya akasema.