• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Uvumi majani chai yanaponya corona wasisimua Pwani

Uvumi majani chai yanaponya corona wasisimua Pwani

Na MISHI GONGO

WAKAZI wa maeneo mbalimbali ya Pwani jana waliamkia kunywa chai bila maziwa na sukari kabla ya jua kuchomoza, kwa imani kuwa inasaidia kuzuia kuambukizwa virusi vya corona.

Hii ni baada ya uvumi kuenea kuwa mnamo Jumamosi usiku kuna mtoto ambaye mara baada ya kuzaliwa alimwambia mama yake awaeleze watu kunywa chai hiyo ili kuwakinga dhidi ya corona.

Kulingana na habari ambazo zilisambazwa kwa simu na mitandao ya kijamii usiku wa Jumamosi, mtu anapaswa kuamka kabla ya jua kuchomoza, kisha ainjike maji na kuyatia majani na kuacha yachemke kwa dakika kadhaa kisha kunywa.

Chai hiyo pia inapendekezwa kuwa sharti ipikwe kwenye jiko la kuni na kutumia sufuria iliyo na masizi ili iweze kuwa na ukali unaohitajika.

“Nilipokea simu kutoka kwa jirani kuwa mtoto alizaliwa usiku wa Jumamosi na ameagiza watu kunywa chai ya rangi kabla ya jua kuchomoza ili kujikinga na corona,” akasema Bi Khadija Athman mkazi wa Likoni.

Japo hakuna mtu anayejua sehemu halisi aliyozaliwa mtoto huyo, wakazi kutoka maeneo mbalimbali yakiwemo Mombasa, Kwale na Kilifi jana waliamka na kutekeleza sharti hilo.

Habari zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zilieleza kuwa baada ya mtoto huyo kumwambia mama yake maneno hayo, aliaga dunia huku wengine wakidai kuwa alitoweka.

Watu wengine nao walieneza uvumi kuwa mtoto huyo alizaliwa akiwa na meno 36, kinyume na mtoto wa kawaida ambaye huwa hana meno.

Katika eneo la Kinango, Kaunti ya Kwale, Samuel Kazungu aliambia Taifa Leo kuwa wafanyabiashara jana walilazimika kufungua maduka yao mapema kuliko kawaida ili kuwauzia wakazi majani chai.

“Katika kijiji chetu, baada ya kupata habari hizo, tuliamshana na kupika chai mapema na kuinywa,” akasema Bw Kazungu.

Bi Esha Shaban kutoka eneo la Mailand Magongo, alisema alibishiwa mlango saa saba usiku na kupashwa habari hizo.

Wiki iliyopita, uvumi ulienea kuwa ndani ya Koran kuna nywele ambayo waumini wa dini ya Kiislamu walipaswa kuitia ndani ya maji kisha kunywa, ili kujikinga na virusi vya corona, jambo ambalo lilipingwa vikali na viongozi wa dini hiyo.

Katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK), Sheikh Mohammed Khalifa alisema uvumi unaoenezwa ni wa kupotosha na hivyo kuna haja ya wakazi kuelimishwa zaidi kuhusu ugonjwa huo.

“Uvumi unaoendelea unaweka nchi yetu mahali pabaya katika kukabiliana na ugonjwa huu,” akasema Sheikh Khalifa.

You can share this post!

Genge laiba bunduki za polisi wakati wa kafyu

Mbunge apata virusi wengine wakimulikwa

adminleo