• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Kongamano la Ugatuzi: Wajumbe wakerwa na kujikokota kwa usajili

Kongamano la Ugatuzi: Wajumbe wakerwa na kujikokota kwa usajili

BENSON AMADALA na DERRICK LUVEGA

WAJUMBE na Wageni wanaohudhuria Kongamano la Ugatuzi katika Kaunti ya Kakamega walilalamikia kujikokota kwa shughuli za usajili iliyokuwa ikiendeshwa katika shule ya Msingi ya Amalemba.

Kufikia saa tano mchana mchakato mzima wa usajili haukuwa umeanza japo baadhi ya wajumbe walikuwa wamefika shuleni humo saa 12 asubuhi.

Maafisa wa Polisi ambao walikuwa wakishika doria walikuwa na wakati mgumu kuwatuliza wajumbe hao, waliokuwa wameanza kukasirikia kujikokota kwa shughuli hiyo.

Nancy Adhiambo ambaye ni Mwakilishi kutoka Kaunti ya Kisumu alilinganisha kushiriki usajili huo na kujihangaisha.

“Baraza la Magavana lingefanya matayarisho ya mapema ili kuhakikisha usajili huu unaendeshwa kwa njia ya haraka. Nimekuwa nikisimama hapa kwa muda wa saa mbili lakini hakuna cha maana kinachoendelea,” akasema Bi Adhiambo.

Naye mwenzake ambaye ni mwakilishi wa Khwisero kutoka Kaunti hiyo Lawrence Oyando aliwataka waandalizi kuharakisha usajili ili wajumbe na wageni wasikose kufuata ratiba yao vilivyo.

“Kinachoendelea kinasikitisha lakini tunatumai hali itaimarika na usajili uharakishwe,” akasema.

Mkazi wa Kakamega Johnson Wandera hata hivyo alisema kwamba hali hiyo ilitokana na waandalizi kutowaelekeza wageni vizuri.

Barabara zinazoelekea eneo la usajili zilishuhudia msongamano mkubwa huku maafisa wa polisi wakiweka vizuizi kwa ukaguzi na kuhakikishia wageni usalama wao.

Afisa Mkuu wa Polisi wa Kakamega Kusini Bernstein Shari alisema maafisa wake wanajukumu kubwa kuhakikisha usalama katika eneo la usajili.

“Tunashirikiana kwa karibu na maafisa kuhakisha usajili unaendelea bila kutatizika. Tunawaomba wageni wawe na subira mafisa wetu wanapojitahidi kuweka vifaa vya kuharakisha usajili,” akasema.

Usalama ulikuwa wa hali ya juu katika uwanja mdogo wa ndege wa Kakamega huku wachezaji wa ngoma za kitamaduni wakiwaburudisha wageni waliokuwa wakiwasili.

Ndege kutoka kitengo cha Jeshi la wanahewa ilitua uwanjani humo saa tano mchana kwa majaribio katika juhudi za kudumisha usalama angani kwa wanaoshiriki kongamano hilo.

Kaunti ya Kakamega ni ya tano kuandaa kongamano la magavana, baada ya la kwanza kuandaliwa katika hoteli ya Leisure Lodge, Diani kaunti ya Kwale.

Kongamano la pili lilikuwa katika kaunti ya Kisumu kisha la tatu likawa Meru na mwaka jana kongamano la nne lilikuwa Kenya Wildlife Training Institute mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.

 

 

 

You can share this post!

Raila anadi upatanisho kwa jamii ya Waluo

Karua ataka korti iagize upya vifaa vya kura Kirinyaga...

adminleo