• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wajumbe 3 wa mapatano

Wajumbe 3 wa mapatano

NA CHARLES WASONGA

JUHUDI za kuanzisha mazungumzo baina ya Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga zinaposhika kasi, imefichuka kuwa viongozi watatu mashuhuri barani Afrika ni kati ya wanaopendekezwa kuongoza mapatano hayo.

Duru za kuaminika zinaeleza viongozi hao, wanaopendekezwa na jamii ya kimataifa kwa mapatano, ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

Ingawa Msemaji wa Ikulu, Hussein Muhamed amekana madai kuwa Rais Suluhu alikuja nchini kama mtalii wala si kwa mwaliko wa Rais Ruto kuongoza mapatano, Bw Odinga amedai kuwa kiongozi huyo wa Tanzania alifika nchini kwa mwaliko wa Rais Ruto ili kuongoza maridhiano kati yao.

Hata hivyo, dalili kuwa Rais Ruto na Bw Odinga hatimaye watakubali kupatana ilijiri Jumanne baada ya Kiongozi wa Taifa kumwalika Bw Odinga kwa mazungumzo.

“Rafiki yangu Raila Odinga. Nimeondoka naelekea Tanzania kwa mkutano kuhusu upanuzi wa nafasi za ajira kwa bara letu. Nitarejea kesho jioni na unavyofahamu kila wakati huwa niko tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana nawe wakati utakaokufaa,” Rais Ruto akasema kupitia ujumbe wa Twitter.

RAMAPHOSA

Hata hivyo, Bw Odinga alidai ujumbe kupitia Twitter sio njia rasmi kwa Rais Ruto kumwalika kwa mazungumzo.

Mbali na Rais Suluhu, kinara huyo wa ODM pia amedai kuwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alikuwa amejitolea kusimamia mazungumzo kati ya mrengo wake na ule wa Rais Ruto. Lakini alidai kuwa Rais Ruto alimkataa Rais Ramaphosa.

“Ninasisitiza kuwa sharti kuwepo mtu kati yetu. Rais Ramaphosa alitaka kuja lakini yeye (Ruto) akakataa,” Odinga akanukuliwa na AFP akisema Jumatano.

Rais Ramaphosa amekuwa rafiki wa muda mrefu wa Bw Odinga.

Mnamo 2008 wakati wa mzozo wa kisiasa uliochochewa na ubishi kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Kofi Annan alimteua Ramaphosa kuongoza mazungumzo ya kuleta amani.

Hata hivyo, licha ya kiongozi huyo kuwa na tajriba ya kuongoza maridhiano, mrengo wa serikali ukiongozwa na marehemu Mwai Kibaki ulimkataa.

Mrengo huo wa chama cha Party of National Unity (PNU) ulidai kuwa Rais Ramaphosa ni mshirika wa kibiashara wa Bw Odinga.

Mnamo 2017, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Bw Odinga walihudhuria sherehe ya kutawazwa kwa Ramaphosa kuwa Rais wa Afrika Kusini.

Kwa upande wake, Bw Olusegun alitumwa nchini Kenya na Umoja wa Mataifa (UN) kuongoza shughuli za kutatua mzozo wa kisiasa.

“Tumekuwa tukifuatilia hali ya kisiasa nchini Kenya kwa ukaribu zaidi hasa kufuatia mipango ya Upinzani kuongoza sherehe ya kuapishwa kwa Bw Raila mnamo Januari 2018. Hii ndiyo maana Katibu Mkuu (Antonio Guterres) alimwomba Obasanjo kuzuru Kenya. Hii ni kwa sababu yeye ni mwanachama wa Jopo la Utapatanishi katika Afisi ya Katibu Mkuu,” akasema Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Bw Guterres.

Hata hivyo, kutokana na sababu ambazo hazikubainishwa, Bw Obasanjo hakutekeleza wajibu huo.

Bw Obasanjo aliongoza Nigeria kati ya Mei 29, 1999 na Mei 29, 2007.

Amekuwa mwandani wa karibu wa familia ya Bw Odinga, tangu enzi ya babake, Jaramogi Oginga Odinga. Katika miaka ya hivi karibuni Bw Obasanjo alishiriki katika mchakato wa upatanisho kati ya serikali ya Ethiopia na kundi la waasi la Tigray (TPLF).

Lakini duru zilisema kuwa baadhi ya wafuasi wa kundi hilo la waasi walidai kuwa Bw Obasanjo alipendelea upande wa serikali ya Ethiopia inayoongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Licha ya madai kuwa Rais Suluhu alialikwa na Rais Ruto kuongoza mazungumzo ya maridhiano, rais huyo aliyetwaa hatamu za uongozi 2021 hana historia ya kuwa mpatanishi katika mzozo wa kisiasa katika taifa lolote duniani.  

  • Tags

You can share this post!

Wapwani wamtunuka sifa Rais Ruto

Manchester United hoi Arsenal ikifinya Barca kirafiki

T L