Habari Mseto

Wazee wataka mitishamba itumike kutibu corona

April 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MAUREEN ONGALA na FLORAH KOECH

WAZEE wa Kaya katika eneo la Pwani, wanaitaka serikali ijaribu kutibu virusi vya corona kupitia mitishamba.

Wazee hao wameeleza kuwa dalili za virusi hivyo ni sawa na za ugonjwa wa ‘Kivuti’ uliokuwepo katika enzi za zamani, na uliotibiwa kwa mitishamba.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitamaduni cha Wilaya ya Malindi (MADICA) Bw Jospeh Mwarandu, ambaye ni mmoja wazee hao, alisema kuwa ni lazima serikali itumie njia tofauti kukabili virusi hivyo.

“Tuko tayari kujaribu matibabu kwa watu ambao wameambukizwa virusi. Hata hivyo, lazima tupate msaada tunaohitaji na vifaa vya kujikinga ili tusiambukizwe,” akasema Bw Mwarandu.

Alisema kuwa ugonjwa wa ‘Kivuti’ ulikuwa ukitibiwa kwa mchanganyiko wa mizizi, matawi na ngozi kutoka kwa aina mbalimbali za miti.

Aliyeugua ugonjwa huo alikuwa na dalili kama homa, kupiga chafya, kuumwa na mapafu na kushindwa kupumua vyema.

Alieleza kuwa mgonjwa angefariki baada ya siku sita ikiwa hangepata matitabu ya haraka.

Alisema kwamba wagonjwa waliokuwa wanaugua maradhi hayo walitengwa na familia zao na jamii, kwani ulikuwa wa kuambukizana.

Kwingineko, wazee wa jamii ya Tugen katika kijiji cha Cheplaot, Mogotio, Kaunti ya Baringo wameanza kufanya matambiko ya kitamaduni ili kulaani virusi vya corona.

Wazee hao na wanawake zaidi ya 20 walianza harakati za kutafuta usaidizi kutoka kwa mababu zao, ili kukabili virusi hivyo ambavyo vimewaua zaidi ya watu milioni kote duniani.

Walisema kuwa ni kupitia matambiko hayo ambapo watawarai miungu wao ili kuiokoa dunia dhidi ya “maradhi hayo yasiyoeleweka.”

Maombi hayo yalifanywa katika mlima mdogo mtakatifu, yakiongozwa na mzee wa kitamaduni aliyebeba kibuyu, maziwa, asali na miti aina ya minazi huku wakiomba kwa lugha ya Kitugen.

Kwenye maombi, wazee waliwarai mababu zao kuwasamehe dhambi zao na kuiokoa dunia dhidi ya corona.

Wakiongozwa na Mzee Kigen Kiptoo, walisema waliona kwamba huenda virusi hivyo vikaiangamiza dunia nzima ikiwa hakuna hatua za haraka zitachukuliwa kuwaokoa watu.

“Tumefahamu kuwa maradhi hayo hayana tiba na huenda yakakimaliza kizazi cha sasa ikiwa hakuna hatua za haraka zitakazochukuliwa. Tunawaamini mababu zetu, kwani wakati kunapokuwa na kiangazi, huwa tunaomba na mvua hunyesha. Tunaamini kuwa miungu watatuokoa ikiwa tutaomba,” akasema Bw Kiptoo.