• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
“Nimezoea maisha ya kafyu, biashara si mbaya vile’

“Nimezoea maisha ya kafyu, biashara si mbaya vile’

Na GEOFFREY ANENE

KAFYU inayolenga kuzuia uenezaji wa virusi vya corona imeathiri vibaya sekta nyingi za maisha kote duniani.

Huku wanafanyabiashara wengi wakilia mambo hayawendei vyema, hata hivyo, kuna wale ambao mambo si mabaya sana kwao jinsi ‘mama mboga’ Margaret Mbatha alisimulia Taifa Leo katika mahojiano mtaani Kariobangi South Civil Servants jijini Nairobi, Jumamosi.

“Sijaona bidhaa yoyote ambayo tumekuwa tukiuzia wateja wetu ambayo imepungua ama kupotea sokoni. Cha kushangaza ni kuwa mboga ya sukumawiki sasa iko kwa wingi. Kabla ya shule zifungwe kwa sababu ya hofu ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona, sukumawiki ilipelekwa katika shule. Shule nyingi huandalia wanafunzi sukumawiki kwa hivyo soko halikuwa na mboga hizi kwa wingi,” anasema Mbatha, ambaye alianzisha biashara hiyo yake mwaka 2005.

Anasema kuwa huenda nje ya Nairobi bei ya sukumawiki ikawa imepanda kwa sababu ya vikwazo vya kupunguza shughuli za wasafiri zinafanya malori mengi yanayoleta bidhaa sokoni kumalizia safari yao Nairobi.”

Aidha, Mbatha amekiri kuwa bei ya bidhaa fulani zimepanda kwa mfano kabeji kubwa sasa ni Sh70. Kabla ya kafyu kuanza anasema alinunua kabeji kubwa kwa Sh50. “Nimeathirika tu kidogo, lakini mabadiliko tu ni bei ya bidhaa kadhaa sokoni, lakini zinapatikana bila shida yoyote.”

Mbatha, 39, hufungua kibanda chake saa tano na nusu asubuhi baada ya kuenda katika mojawapo ya soko kubwa jijini Nairobi, soko la Korogocho. Yeye huenda sokoni kila siku kununua bidhaa anazomaliza kuuza siku hiyo.

Kabla ya kafyu, Mbatha, ambaye ni mzawa wa mji wa Mombasa, alikuwa akifunga biashara saa nne, lakini sasa saa moja jioni inapata amefunga kazi na kuingia kwenye nyumba.

Kuhusu idadi ya wateja, Mbatha, ambaye aliacha kusoma katika darasa la tano kwa sababu ya matatizo ya karo, anasema, “Wateja wamepungua. Wengi walikuwa wanapatikana saa moja usiku, lakini sasa huwezi kuwapata kwa sababu huo ndio wakati kafyu inaanza.”

Kafyu hiyo ya nchi nzima inayoanza saa moja usiku hadi saa kumi na moja asubuhi kila siku, ilitangazwa na Machi 27. Inalenga kupunguza shughuli za Wakenya usiku zilizoaminika kuchangia katika maambukizi zikiwemo maombi ya usiku makanisani almaarufu kesha, burudani katika mabaa na maeneo mengine ya burudani na mikusanyiko ya watu wengi.

Serikali ilitangaza siku mbili zilizopita kuwa huenda ikalazimika kuongeza saa za kafyu hiyo kwa sababu Wakenya hawafuati amri walizoagizwa kufuata ikiwemo kuepuka mikusanyiko ya watu wengi na pia kukaa nyumbani.

Ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ulianzia mjini Wuhan nchini Uchina mapema mwaka huu na kusambaa dunia nzima. Walioambukizwa kote duniani ni zaidi ya 1,000,000. Kenya imethibitisha visa 126 na vifo vinne.

You can share this post!

Msaada kwa wakazi wa Westlands

CORONA: Mkenya anayeishi Italia asimulia maisha...

adminleo