Makahaba wataka wawekwe kwa orodha ya wanaotoa huduma muhimu!
Na Wachira Mwangi
HOFU ya kufa njaa imewakumba makahaba katika Kaunti ya Mombasa na sasa wanataka wajumuishwe miongoni mwa watu wanaotoa huduma muhimu, la sivyo, wapewe chakula cha msaada.
Makahaba hao walisema kuwa kufungwa kwa baa, hoteli na maeneo mengine ambapo walikuwa wanapata kipato, na pia watalii kuzuiliwa kuingia nchini, sasa kumewakosesha kipato kabisa.
Walisema pia tangu marufuku ya kutotoka nje usiku iwekwe ili kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona, maisha yamezidi kuwa magumu kwa kuwa hawana wateja.
Afisa wa sheria kutoka Changamwe, Bi Betty Kitili, alisema kuwa makahaba hawana muda wa kutosha kufanya kazi zao mchana na pia malipo ni duni.
“Bado tunahitajika kulipa kodi za nyumba, kununua vyakula na kufanya mambo mengi ambayo yanahitaji pesa. Ninaona hatutakufa kwa corona, ila njaa ndiyo itakayotumaliza,” akasema Bi Kitili.
Mwenyekiti wa shirika la High Voice Africa, Bi Maryline Laini, alisema wengine wanalipwa Sh20 pekee ili angalau wakanunue chakula.
“Asilimia 90 ya makahaba sasa hawana kazi. Majengo kama vile baa, hoteli na klabu yamefungwa. Hizo ni sehemu ambazo wengi wetu tulipata riziki,” akasema Bi Laini.