Buriani mwanasafu mwenza Ken Walibora – Bitugi Matundura
NA BITUGI MATUNDURA
KIPINDI kati ya miaka ya 1980 hadi 1990 kilikuwa ni kipindi kigumu mno kwa fasihi ya Kiswahili kwa jumla na hususan utanzu wa riwaya nchini Kenya.
Hali hii ilitokana na ukweli kwamba ni Wakenya wachache mno – waliokuwa wakitunga kazi za fani hizo. Hali hii ilisababisha wahakiki wa fasihi kudai kwamba ‘fasihi ya Kiswahili ilikuwa imedumaa’.
Katika kipindi hicho, Taasisi ya Elimu ya Kenya (Sasa Taasisi ya Ukuzazi wa Mitaala ya Kenyayaani KICD) ilitegemea sana vitabu vya fasihi vilivyotungwa na Watanzania – kutahiniwa katika mifumo yetu ya elimu.
Hata hivyo, katikati ya mwaka 1990, ustawi wa fasihi ya Kiswahili ulipata msukumo na nguvu mpya wakati waandishi wa Kenya walipojitosa ulingoni. Miongoni mwa watunzi hao walikuwa ni Ken Walibora – ambaye riwaya yake – Siku Njema iliteuliwa kutahiniwa kama kitabu cha lazima katika mtihani wa KCSE.
Tangu wakati huo, mwandishi huyu ambaye pia alikuwa msomi mahiri amechapisha tungo nyingi katika mapana na marefu ya tanzu zote za fasihi ya Kiswahili. Katika Afrika ya Mashariki, sikosei kudai kwamba ni waandishi watatu tu ambao wamefanikiwa kandika tungo za Kiswahili zilizotamba katika tanzu zote za fasihi – riwaya, tamthilia, hadithi fupi, ushairi, novela na fasihi ya watoto. Waandishi hao ni pamoja na Ken Walibora, Said Ahmed Mohamed na Kyallo Wadi Wamitila.
Haiyumkiniki kusema kila kitu kumhusu Prof Kennedy Atanasi Waliaula – ambaye jina lake la uandishi lilikuwa ni Ken Walibora kwa sababu alikuwa ni mja aliyekirimiwa vipawa vingi. Maisha yake yalizunguka katika vitovu vikuu vinne – uanahabari, usomi, uandishi na ualimu.
Licha ya kubobea katika nyanja hizi, alifahamika mno katika ulingo wa uandishi – hasa utanzu wa riwaya. Riwaya yake maarufu ni Siku Njema ambayo inafumbata kwa uketo taswira ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa. Riwaya hii inaweza kuainishwa kuwa kazi bulibuli (classical). Imetafsiriwa kwa Kiingereza na Kiitaliano.
Riwaya zake nyingine ni Kidagaa Kimemwozea, Ndoto ya Almasi, Kufa Kuzikana. Tawasifu yake, Nasikia Sauti ya Mama inaonesha hulka na changamoto alizopitia kufikia kilele cha juu kabisa katika uanahabari, usomi na uandishi.
Nilifahamiana na Prof Ken Walibora mnamo 2003 nilipokuwa mhariri wa habari katika Shirika la Habari la Kenya (KBC). Tangu kipindi hicho, tumekuwa tukitagusana katika nyanja za taaluma ya uanahabari, uandishi wa vitabu na usomi. Mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Machi 5, 2020 ambapo nilimuuliza anipe fasiri ya neno ‘anihilate’.
“Prof kwema? Naomba tafsiri ya ‘anihilate’. Nimeangukia kitu hapa,’’ nikamuuliza.
Kauli hii ilitokana na makala aliyokuwa ameyaandika katika Taifa Leo akikejeli watu wanaovuruga Kiswahili kwa kutafsiri vibayavibaya.
Prof Walibora alikuwa mwalimu pia. Mbali na kufundisha katika chuo kikuu cha Wisconsin – Madison Marekani, alikuwa pia mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Riara. Tunaweza kudai kuwa alikuwa mwalimu wa jamii pana kutokana na tungo zake za kifasihi.
Taifa Leo
Kwa takriban miaka minne, tumekuwa tukiandika safu ya Kina cha Fikra katika Gazeti la Taifa Leo. Amewahi pia kupendekeza kwamba wanafunzi wa uzamili na uzamifu katika vyuo vikuu wachangamkie utafiti wa makala katika Jarida la Lugha la Elimu katika gazeti la Taifa Leo.
Prof Walibora kwa hakika alikuwa mmoja wa wanariwaya bora zaidi kuwahi kuibukia Afrika ya Mashariki. Mchango wa marehemu Ken Walibora utaendelea kuacha taathira kubwa katika tasnia ya Kiswahili.
Prof Walibora amekwisha kutangulia mbele za haki. Kinachoridhisha mioyo yetu na kutupa ukakamavu na ujasiri wa kuendelea kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Kiswahili ni kwamba watu sampuli yake hutokea mara mojamoja katika kizazi – na gurudumu la maisha haliwezi kusimama. Hatahitaji kujengewa minara ya kumbukumbu.
Mchango wake katika ulingo wa fasihi ya Kiswahili utadumu daima dawamu. Kawape salamu zangu kina Muyaka Al-Ghassanny, Hassan Mwalimu Mbega, Seithy Chachage, Omar Babu, Katama Mkangi, Jay Mashanga Kitsao, Mumamed Said Abdulla, Ben Rashid Mutobwa, Mbunda Msokile, Shabaan bin Robert, Catherine Kisovi, Mzee Sheikh Ahmad Nabhany, Ibrahim Ngozi miongoni mwa waandishi wengine wengi. Buriani ndugu Walibora.
Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili Katika Chuo Kikuu cha Chuka.