Ligi Kuu Uholanzi yafutwa, hakuna mshindi
Na CHRIS ADUNGO
LIGI Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) imefutiliwa mbali msimu huu na kwa sasa hapatakuwepo mshindi wala kikosi kitakachoshushwa ngazi.
Maamuzi hayo yanachochewa na hatua ya serikali ya Uholanzi kupiga marufuku shughuli zote za michezo nchini humo hadi Septemba 1 ili kukabiliana vilivyo na janga la virusi vya corona.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Uholanzi (KNVB), itakuwa vigumu zaidi kwa sasa kuandaa mashindano yoyote katika juhudi za kukamilisha kampeni za msimu huu.
Hadi kufutiliwa mbali kwa msimu huu mzima wa Eredivisie, Ajax walikuwa wamejizolea jumla ya alama 56 zilizowaweka kileleni mwa jedwali kutokana na mechi 25.
AZ Alkmaar waliokuwa pia wamejizolea alama 56 walikuwa katika nafasi ya pili kutokana na uchache wa mabao. Feyenoord walikuwa katika nafasi ya tatu kwa alama 50, moja pekee kuliko PSV Eindhoven waliofunga orodha ya nne-bora katika jedwali la vikosi 18.
Ilivyo, Ajax na Alkmaar watafuzu kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, japo suala hilo litasubiri kurasimishwa na vinara wa mapambano hayo ya haiba kubwa.
Hakuna kikosi chochote kitakachopandishwa wala kuteremshwa daraja kwa minajili ya msimu ujao. Hatua hii inamaanishwa kwamba kikosi cha Cambuur kilichokuwa kikijivunia pengo la alama 11 kileleni mwa Ligi ya Daraja ya Kwanza hakitakwezwa ngazi kuwania ufalme wa Eredivisie msimu ujao.
Katika mahojiano yake na runinga ya NOS nchini Uholanzi, kocha Henk de John wa Cambuur alissisitiza kwamba maamuzi ya kufutilia mbali msimu huu wote wa Eredivisie ndiyo ya “kusikitisha zaidi katika historia ya soka ya taifa hilo”.
Kwa upande wao, KNVB walisema: “Tunajua kwamba hatua fulani ingelazimu kuchukuliwa na matokeo ya kila hatua yangeumiza mhusika fulani mahali fulani.”
“Itakuwa vyema iwapo washikadau wote kuanzia kwa mashabiki, wachezaji, wakurugenzi na marefa wa Eredivisie wataelewa kwamba afya ya umma siku zote ndiyo inayostahili kuja kwanza,” ikasema sehemu ya taarifa ya shirikisho hilo.
Kufikia jana, zaidi ya watu 4,000 walikuwa wameaga dunia kutokana na virusi vya corona nchini Uholanzi.
Ni mara ya kwanza tangu 1956 kwa msimu wa Eredivisie kukamilika bila ya timu yoyote kutawazwa mshindi. Katika taarifa yake, KNVB ilishikilia kwamba isingewezekana kupandisha ngazi kikosi chochote kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza bila ya kikosi chochote kushushwa daraja kutoka Eredivisie.
Kabla ya kufikia maamuzi hayo, KNVB ilisema kwamba ilishauriana kwa kina na wadau wote ambao pia hawakuafikiana walipopewa fursa ya kupiga kura ambayo matokeo yake yangeamua iwapo vikosi vya mwisho katika Eredivisie vingeteremshwa ngazi huku vya kwanza katika Ligi ya Daraja ya Kwanza vingepandishwa daraja.
“Wadau walikuwa wapige kura ya “hakuna kushuka daraja wala kupanda daraja” au “kuna kushuka daraja na kupanda daraja”.
Baada ya matokeo kuonyesha kwamba kila upande ulikuwa na idadi sawa ya kura, KNVB iliamua kuingilia kati na kufikia maamuzi ya kutopandisha ngazi wala kuteremsha daraja kikosi chochote.
“Hapakuwepo na utaratibu mwafaka kupandisha daraja klabu zozote wala kuteremsha ngazi vikosi vyovyote kwa sababu hadi kufutiliwa mbali kwa msimu huu, kulikuwa bado na raundi nyingi za kuchezwa na washiriki kabla ya muhula kukamilika,” ikasema taarifa ya KNVB.
Feyenoord watafuzu sasa watafuzu kushiriki hatua ya makundi ya Europa League msimu ujao huku PSV na Willem II wanaoshikilia nafasi za nne na tano mtawalia wakifuzu kwa mchujo wa kivumbi hicho iwapo wataidhinishwa na Uefa.
Kwa upande wa wanawake, Ligi Kuu ya Eredivisie pia imekamilika bila mshindi huku PSV wakipokezwa tiketi ya kushiriki kipute cha UEFA nao Ajax ambao wanashikilia nafasi ya pili jedwalini wakijikatia tiketi ya mchujo.