Kampuni ya Capwell Thika yaweka mikakati ya kukabiliana na corona
Na LAWRENCE ONGARO
KAMPUNI ya Capwell Ltd mjini Thika imetoa mchango wake ili kuungana na mashirika mengine kusaidia vita dhidi ya janga la corona.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Bw Rajan Shah, amesema kampuni yake kwa njia ya kipekee imetoa Sh20 milioni ili kujumuishwa katika hazina ya Covid-19 Fund.
“Kati ya fedha hizo Sh2 milioni zitasaidia Kaunti ya Kiambu kulinda dhidi ya janga hilo. Sisi kama kampuni tunafanya hivyo ili kupunguza makali ya janga hilo kwa njia moja ama nyingine,” alisema Bw Shah.
Amesema licha ya hali ngumu ya mambo, kiwanda chake cha wafanyakazi 650 kinaendelea na shughuli kama kawaida.
“Hatungetaka kuona wafanyakazi wetu wakiregeshwa nyumbani kwa sababu ya janga hilo kwa sababu tunajali maslahi yao na familia zao,” amesema Bw Shah.
Amesema mambo muhimu ambayo wanazidi kuhimiza ni kudumisha usafi , kuvalia barakoa, na kuweka nafasi kiasi kando ya mwenzako.
Ameyasema hayo Alhamisi alipohutubia waandishi wa habari afisini mwake mjini Thika akiwajulisha hatua walizochukua kwa muda huo wa mwezi mmoja ambao umepita.
Amesema hata ingawa wanazidi kupambana na kuendesha kazi yao, biashara imerudi chini kufuatia mlipuko wa homa hiyo ya corona.
Kiwanda hicho kwa kawaida kinapakia unga chapa Soko kwenye karatasi na pia mchele wa gredi ya kwanza, pamoja na kupakia bidhaa za maiziwa chapa ya Yola.
Anasema kiwanda chake kinajali jamii vijijini na ndiyo maana wamesambaza matangi ya maji katika vijiji kadhaa vya mji wa Thika.
“Tunasaidia wasiojiweza na wakongwe na chakula na sabuni ili waweze kunufaika wakati huu wa kupambana na janga la corona.
Amesema kama wafanyabiashara wanapitia masaibu mengi kwa sababu homa ya corona imevuruga biashara kwa kiwango kikubwa na kwa hivyo wanalazimika kutumia mbinu nyingi kuona ya kwamba bado wanasimama katika ulingo huo.
“Tukiungana pamoja kama Wakenya tutaliangamiza janga hilo ambalo limetikisa ulimwengu mzima bila huruma,” akasema mkurugenzi huyo.
Ameongeza cha muhimu kwa sasa ni kuona ya kwamba wanafuata maagizo yote ya serikali ya kuona ya kwamba watu wananawa mikono kila mara kwa sabuni, kuvalia barakoa, na cha muhimu zaidi ni kutengana kwa mita chache baina ya mtu na mwenzake.
“Hata mimi hapa kama kinara nimeweka mikakati mikali ambapo unapoingia kiwandani, ni sharti upimwe halijoto ya mwili katika lango kuu, halafu unanawa mikono. Ni lazima mgeni yeyote kuvalia barakoa kabla ya kuruhusiwa kuingia ndani ya kiwanda hiki,” amefafanua Bw Shah.