Uhuru aundiwa chama kipya?
Na WANDERI KAMAU
IMEIBUKA kwamba mabwanyenye katika eneo la Mlima Kenya wanapanga kukitumia chama cha PNU kuwa “dau mpya” la eneo hilo kwenye uchaguzi wa 2022, ikiwa Chama cha Jubilee (JP) kitasambaratika.
Wadadisi pia wanataja hilo kama mkakati wa Rais Uhuru Kenyatta “kumnyang’anya” Naibu Rais William Ruto udhibiti wa kisiasa katika eneo hilo, ambalo ni ngome yake.
Duru zinaeleza kuwa mipango ya kukibadili jina chama hicho kuwa The National Unity Party (TNU) tayari iko karibu kukamilika na usajili wake rasmi kukabidhiwa Afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa.
Kulingana na ripoti, mabwanyenye hao walikutana katika hoteli moja viungani mwa jiji la Nairobi wiki iliyopita, ambako mchango mfupi wa kufadhili shughuli za chama hicho kipya ulifanyika.
Baadhi ya viongozi wakuu serikalini waliohudhuria ni Waziri wa Kilimo Peter Munya, kwani ndiye amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa sasa.
Na kutokana na hatua hiyo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa huenda hilo likawa mojawapo ya hatua za kichinichini za Rais Kenyatta na waandani wake wa karibu kisiasa katika Chama cha Jubilee (JP) kubuni mkakati watakaofuata kisiasa, ikiwa mustakabali na uthabiti wa JP utaendelea kuyumba kama ilivyo sasa.
Vilevile, wanataja hali hiyo kama “plan B” ya Rais kwenye mpango wa kubuni muungano wa kisiasa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, Seneta Gideon Moi katika Kanu miongoni mwa wanasiasa wengine.
Kulingana na Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, huenda isiwe furaha ya Rais Kenyatta kubuni muungano huo chini ya mazingira ya mafarakano na hali ya kutoelewana kama ilivyo sasa katika Jubilee.
“Si kwamba Rais Kenyatta hashuhudii wala hafuatilii yanayoendelea katika Jubilee. Yeye ni mwanasiasa, ambaye licha ya muda wake kuhudumu kukaribia kuisha, lazima atazame mbele kwa kubuni mazingira, ambapo yeye, familia yake na washirika wake kisiasa watakuwa salama chini yake,” asema Prof Munene.
Wadadisi wanaeleza kuwa kwa kuwashirikisha tena mabwanyenye na watu maarufu kwenye usajili mpya wa PNU, viongozi wakuu katika Mlima Kenya, akiwemo Rais Kenyatta, wanalenga kuanza kukinadi kama “dau” litakalotumika na eneo hilo kufanikisha mipango ya kubuni muungano wa kisiasa na Odinga, Moi miongoni mwa viongozi wengine.
Wanataja hilo kama njia ya pekee kwa Rais Kenyatta kuchukua mwelekeo mpya kisiasa, ikiwa “itakuwa vigumu kwake kutwaa udhibiti” wa Jubilee kutoka kwa Dkt Ruto na waandani wake kisiasa.
Kumekuwa na makabiliano makali kati ya waandani wa Rais na Dkt Ruto kuhusu udhibiti wa Jubilee, pande zote zikiapa kufanya kila ziwezalo “kutetea maslahi yao chamani.”
Waandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimlaumu Katibu Mkuu, Bw Raphael Tuju na Naibu Mwenyekiti, Bw David Murathe, kwa kuendesha njama za kichinichini kumwondoa Dkt Ruto kwenye udhibiti wa chama hicho.
Na kama Rais Kenyatta, Dkt Ruto pia ameripotiwa kubuni vyama viwili vya siasa, ikiwa atapoteza udhibiti wa Jubilee.
Lakini kufuatia uzinduzi mpya wa PNU, wadadisi wanatilia shaka ikiwa juhudi hizo zitafaulu kufuta dhana ya usaliti wa Dkt Ruto na wandani wa Rais Kenyatta katika eneo hilo.
Hili ni kutokana na mpenyo mkubwa ambao alikuwa amefanya, kabla ya kuzuka kwa janga la virusi vya corona, ambalo limesambaratisha shughuli nyingi za kisiasa nchini.
Wadadisi wanasema kuwa ingawa huo ni mpango mzuri kwa Rais Kenyatta, idadi kubwa ya wakazi bado inaona njama hizo kama mpango wa wazi kumsaliti kisiasa Dkt Ruto.
Wanasema kuwa ni sababu hiyo ambapo huenda iwe vigumu kukiuza upya chama hicho, ikiwa baadhi ya viongozi wanaoonekana “kumpiga vita” Dkt Ruto kama Mabwana Murathe na Tuju watakuwa sehemu ya muundo mpya wa TNU.
“Ikiwa Jubilee hatimaye itasambaratika na TNU kuonekana kama chama kipya kitakachookoa jahazi Mlima Kenya, basi lazima viongozi wa zamani katika Jubilee kama Bw Murathe wasionekane hata kidogo. Hii ni kwa kuwa itafasiriwa kuwa wao ni mwendelezo tu wa njama za kumsaliti Ruto kisiasa,” asema Bw Charles Mulira, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Vilevile, uwepo wa vyama vya kisiasa kama Transformation National Party (TNAP) na The Service Party (TSP) vinavyohusishwa na mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini) na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri mtawalia, pia unatajwa kuwa hali itakayowapa waandani wa Rais Kenyatta ugumu kukiuza chama hicho kipya.
Wawili hao ni waandani wa karibu wa Dkt Ruto na wamekuwa miongoni mwa watetezi wake wakuu Mlimani.
Vyama hivyo vilisajiliwa mapema mwaka huu na tayari vimeanza kuwasajili wanachama na kufungua matawi katika sehemu mbalimbali nchini.
Hata hivyo, baadhi ya watetezi wa Rais Kenyatta wanasema kuwa yeye ni mwanasiasa mwenye tajriba, na haitakuwa mara yake ya kwanza kuacha chama na kubuni safari yake huru kisiasa.
“Rais Kenyatta aliacha Kanu na kubuni TNA mnamo 2012 na kushinda urais mnamo 2013, licha ya masaibu yaliyomwandama kama mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Hivyo, huu ni mtihani rahisi kwake,” asema mbunge wa Kieni, Kanini Keega, ambaye ni mojawapo ya watetezi sugu wa Rais.