KNUT yataka walio karantini shuleni waondolewe
Na FAITH NYAMAI
KATIBU Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Kenya (KNUT), Bw Wilson Sossion, anataka watu waliowekwa karantini katika shule mbalimbali nchini kuondolewa mara moja.
Katibu huyo anataka pia walimu wapewe vifaa kujilinda kuambukizwa virusi vya corona (PPEs) endapo watahitajika kurudi shuleni.
Hata hivyo, alisema kuwa taasisi hizo zinapaswa kufunguliwa tu baada ya kukaguliwa na idara husika na kutangazwa kuwa salama dhidi ya virusi.
“Watu walio katika shule ambazo zimegeuzwa karantini wanapaswa kuondoka ili kuziruhusu kurejelea shughuli zake mara moja baada ya kukaguliwa na maafisa wa afya ya umma,” akasema Bw Sossion.
Bw Sossion alisema kuwa ikiwa shule zitafunguliwa, wasimamizi wake wanafaa kuwapa walimu na wafanyakazi wengine taratibu kamili kuhusu njia za kujilinda dhidi ya kuambukizwa virusi hivyo, angaa siku tatu mapema.
Alitoa kauli hiyo kwenye barua aliyomwandikia Waziri wa Elimu Prof George Magoha mnamo Ijumaa.
Kando na hayo, alisema kuwa shule hizo zinapaswa kuzingatia kanuni zingine muhimu kama kuhakikisha watu hawakaribiani, hasa madarasani na maeneo ya maakuli.
Vile vile, katibu alisema Wizara ya Elimu inapaswa kuhakikisha kuwa mpango wa kuwalisha wanafunzi unarejelewa upya, ili kuwapunguzia wazazi mzigo wa kifedha kukidhi mahitaji ya wanao.
“KNUT inaiomba Wizara ya Elimu kuchukua hatua za haraka kushirikiana na wadau wote wa elimu ili kuhakikisha hali ya usalama imezingatiwa katika shule zimelindwa dhidi ya corona,” akasema.
Uhaba
Kwa upande mwingine, akitoa taarifa mbele ya Seneti, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Vyuo Anuwai (KUPPET), Bw Akelo Misori, alisema kuwa serikali imezigeuza taasisi 460 za elimu kuwa karantini kutokana na uhaba wa taasisi za afya.
Taasisi hizo ni vyuo vikuu na vyuo anuwai 25, vyuo 28 vya mafunzo ya matibabu (KMTC), vyuo 28 vya mafunzo ya walimu na shule 331 za upili.
“Kama chama, hatutaunga mkono hatua yoyote kufungua upya shule hadi pale tutakapothibitisha kwamba janga la corona limedhibitiwa kikamilifu,” akasema.
KUPPET pia imelalamikia pengo kubwa lililopo kati ya wanafunzi kwenye mfumo wa masomo dijitali unaoendeshwa na wizara hiyo.
“Hakuna anayefahamu idadi ya wanafunzi wanaoendelea na masomo yao kikamilifu, kwani hakuna anayenakili masuala muhimu kuhusu hatua za kimasomo wanazofanya,” akasema.