Muungano wa Jubilee na Kanu unalenga kumwondoa Murkomen katika wadhifa wake?
Na CHARLES WASONGA
DURU zinasema huenda mkutano wa maseneta wa Jubilee ambao Rais Uhuru Kenyatta ameitisha katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu utatumiwa kutekeleza mabadiliko katika uongozi wa Seneti, miongoni mwa masuala mengine kuhusu chama hicho.
Wanaolengwa kuvuliwa nyadhifa zao ni Kiongozi wa Wengi Kipchumba Murkomen na Kiranja wa Wengi Susan Kihika ambao wameondokea kuwa ‘wakaidi’ kwa Rais Kenyatta.
Inasemekana kuwa nafasi ya Bw Murkomen huenda ikapewa Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi au Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio.
Na kiti cha Bi Kihika ambaye ni Seneta wa Nakuru huenda kikamwendea Naibu wake Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a.
Haya yanajiri siku ambapo iliripotiwa kuwa chama cha Kanu kimetia saini mkataba wa kubuni muungano wa baada ya uchaguzi na chama tawala cha Jubilee.
Hatua hiyo sasa inamaanisha kuwa maseneta wa Kanu, Mbw Moi, Poghisio na Bi Abishiro Halakhe (Seneta Maalum) watakuwa huru kuhudhuria mkutano wa kundi la maseneta wa Jubilee Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi.
Kulingana na stakabadhi zilizosambazwa mitandaoni na mwandani wa Naibu Rais William Ruto, mwanablogu Dennis Itumbi, stakabadhi za muafaka huo ziliwasilishwa kwa afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (RPP) Anne Nderitu.
Hati hiyo imetiwa saini na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju na mwenzake wa Kanu Nick Salat pamoja na mwenyekiti Seneta Moi (Kanu) na mwenzake Nelson Dzuya.
Hata hivyo, huenda wandani wa Dkt Ruto wanapinga muafaka huo wa muungano kati ya Kanu na Jubilee kwa kuutaja kama unaokiuka Katiba ya chama hicho tawala.
Kulingana na kipenge cha 32 cha Katiba ya Jubilee sharti Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ikutane kuidhinisha pendekezo lolote la kubuniwa kwa muungano na chama chochote cha kisiasa baada ya uchaguzi.