Habari Mseto

Wito serikali iweke vifaa muhimu kwa ajili ya walemavu katika karantini

May 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

WATU wanaoishi na ulemavu mjini Mombasa wameilamu serikali kuu na ile ya kaunti kwa kukosa kutenga vituo vya karantini vyenye vifaa muhimu kwao.

Wakizungumza Jumanne na Taifa Leo walisema vituo vya karantini vilivyoko havijawazingatia.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa shirika la Tunaweza Women with Disability Bi Charity Chahasi, inasikitisha kuona kwamba walemavu wamesahaulika, ikizingatiwa pia wao wako kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Naomba serikali itengeneze vituo ambavyo vinaweza vikatumika na walemavu walioko katika karantini na hata wale vipimo huenda vikabainisha wana maradhi ya Covid-19,” akasema Bi Chahasi.

Ameitaka serikali itenge karantini maalum kwa ajili ya walemavu na vituo hivyo viwe na wahudumu wa afya watakaokuwa wakiwashughulikia walemavu wenye Covid-19.

Alisema kuwa jamii ya walemavu iko katika hatari kuu ya maambukizi kufuatia uhitaji wao watu kuwasaidia katika shughuli na huduma mbalimbali.