• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Wakazi wa mitaa duni hawaamini virusi vinaweza kusambaa kanisani – Utafiti

Wakazi wa mitaa duni hawaamini virusi vinaweza kusambaa kanisani – Utafiti

LEONARD ONYANGO na WANDERI KAMAU

HUKU idadi ya wanaoambukizwa virusi vya corona ikiendelea kuongezeka nchini na hata vifo kuripotiwa, wakazi wa mitaa ya mabanda jijini Nairobi hawaamini virusi hivyo vinaweza kuenezwa katika maeneo ya ibada.

Utafiti huo uliofanywa na kampuni ya TIFA katika mitaa ya Huruma, Kibera, Mathare, Korogocho, Mukuru kwa Njenga na Kawangware, unaonyesha kuwa, asilimia 99 ya wakazi wa mitaa hiyo hawaamini maambukizi ya virusi vya corona yanaweza kutokea kanisani au misikitini.

Hata hivyo, wakazi wa mitaa hiyo wanaamini virusi vya corona vinasambaa kwa kasi katika maeneo mengine yenye msongamano mbali na makanisani au misikitini.

Karibu asilimia 99 pia hawaamini kuwa vyoo au bafu za umma zinaweza kuhusika katika usambazaji wa virusi vya corona.

Idadi kubwa ya wakazi wa maeneo hayo wanaishi kwa hofu kuhusu uwezekano wa kuambukizwa virusi vya corona.

Kulingana na utafiti huo, asilimia 71 wanasema wanahofia kuwa huenda wakapatwa na virusi vya corona.

Hata hivyo, hofu ni nyingi miongoni mwa wanawake ikilinganishwa na wanaume.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa idadi kubwa ya wakazi wa Nairobi wanapendelea kunawa na kuvalia barakoa kama njia mojawapo ya kuepuka kuambukizwa virusi.

“Asilimia 82 ya watu waliohojiwa walisema kuwa, wanapendelea kunawa mara kwa mara ili kuepuka kirusi au virusi kuwepo. Asilimia 79 walisema wanavalia maski huku asilimia 40 wakisema wanakwepa maeneo yenye msongamano wa watu,” unasema utafiti huo uliofanywa kati ya Aprili 25 na 27, 2020.

Kati ya watu 356 waliohojiwa ni asilimia moja pekee waliosema kuwa hawasalimiani kwa mikono au kuepuka kugusa nyuso zao kuzuia kuambukizwa virusi vya corona.

Wakati huo huo, serikali Jumatano iliwaonya vikali vijana waliopewa majukumu ya kudumisha usafi katika maeneo mbalimbali nchini, dhidi ya kuwatoza watu ada za kuwafanyia usafi katika maeneo wanamoishi.

Wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza mpango maalum kuwaajiri vijana zaidi ya 170,000 katika mitaa mbalimbali ya mabanda nchini, kwenye mpango wa kuwasaidia kupata ajira wakati nchi inapokabiliana na janga la virusi vya corona.

Lakini akihutubu Jumatano kwenye kikao cha kila siku kuhusu hali ya virusi hivyo nchini, Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman, alisema kuwa wamepokea malalamishi kuwa baadhi ya vijana wanawatoza fedha wananchi huku wengine wakiwahangaisha waendeshaji magari.

Na kwenye kikao cha Jumatano, idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo ilifikia 737 baada ya watu 22 zaidi kuthibitishwa kuambukizwa.

You can share this post!

COVID-19: Wakazi wengi wa Bonde la Ufa hawazingatii...

Lesotho yathibitisha kisa cha kwanza cha Covid-19

adminleo