• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Serie A kurejelewa rasmi Juni 13

Serie A kurejelewa rasmi Juni 13

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha Ligi Kuu ya Italia (Serie A) sasa kitarejelewa Juni 13, 2020 iwapo serikali itaidhinisha maamuzi ya vinara wa soka la taifa hilo.

Wasimamizi wa soka ya Italia walikutana Mei 13 na kuafikiana kuhusu tarehe ya kuanza upya kwa kivumbi hicho kitakachoendeshwa chini ya kanuni mpya za afya ambazo zimetolewa na serikali ya Italia katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Vikosi vyote 20 vya Serie A vilirejea kambini mapema Mei ila kila mchezaji anajifanyia mazoezi kivyake.

Ligi Kuu ya Italia ilisimamishwa kwa muda mnamo Machi 9 zikiwa zimesalia mechi 12 zaidi za kutandazwa katika kampeni za muhula huu.

Juventus ambao wanafukuzia ubingwa wa taji la Serie A kwa mara ya tisa mfululizo msimu huu wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 63, moja zaidi kuliko Lazio.

Kwa mujibu wa vinara wa soka wa Italia, wanasoka wa vikosi vyote 20 vya Serie A wataanza kushiriki mazoezi ya pamoja kuanzia Jumatatu ya Mei 18, 2020.

Italia ndilo taifa lililoathiriwa zaidi na janga la corona barani Ulaya huku baadhi ya wachezaji wanaonogesha Ligi Kuu ya Serie A wakipatikana na virusi vya homa hiyo hatari.

Wiki jana, wanasoka watatu wa kikosi cha Fiorentina na wafanyakazi watatu wa klabu hiyo ya Serie A walipatikana na virusi vya corona, siku chache baada ya mchezaji mwingine wa Torino kuugua.

Awali, Waziri Michezo wa Italia, Vincenzo Spadafora, alikuwa ameonya kwamba serikali ilikuwa ikiwazia kufutilia mbali msimu huu mzima wa Serie A baada ya Ufaransa kufutilia mbali msimu mzima wa Ligi Kuu ya Ligue 1 na kusitisha zaidi shughuli zote za michezo nchini humo hadi Septemba 2020.

Ingawa hivyo, kinara wa Shirikisho la Soka la Italia, Gabriele Gravina aliapa kutolegeza kamba katika juhudi za kushawishi Serikali kushirikiana na washikadau wote kufanikisha mipango ya kurejelewa kwa kampeni za Serie A muhula huu.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka la Italia (FIGC), kivumbi cha Serie A kimepangiwa kutamatika rasmi kufikia mwanzo wa wiki ya kwanza ya Agosti 2020 na mechi zote zilizosalia zitasakatwa ndani ya viwanja vitupu.

Mbali na Paulo Dybala wa Juventus, wanasoka wengine wa Serie A waliougua corona ni Daniele Rugani, German Pezzella, Patrick Cutrone, Dusan Vlahovic, Manolo Gabbiadini, Omar Colley, Albin Ekdal, Antonio La Gumina, Morten Thorsby, Fabio Depaoli na Blaise Matuidi.

You can share this post!

PAUL THIONG’O: Amewahi kutuzwa zawadi maalum na...

‘Chakula kinauzika sokoni kuliko bidhaa...

adminleo