Habari

Shoka la Uhuru latua Mlima Kenya

May 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

WASHIRIKA wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya, wameingiwa na tumbojoto kufuatia ripoti kuwa shoka la Rais Uhuru Kenyatta sasa linaelekezwa kwao.

Hii ni baada ya kubainika kuwa Rais ameamua kuwazima wanachama wa kundi la ‘Tangatanga’ kwa kuwataka wapigakura kuwafuta kazi.

Mapema wiki hii Rais Kenyatta aliwaondoa wanachama wa kundi hilo, Kipchumba Murkomen na Susan Kihika kutoka nyadhifa za Kiongozi wa Wengi na Kiranja wa Jubilee katika seneti.

Tayari, kama hatua ya kudhihirishia Tangatanga kwamba chuma chao ki motoni, chama hicho kimeanza utaratibu wa kuwaadhibu maseneta watano maalumu waliosusia mkutano ulioandaliwa na Rais katika Ikulu ya Nairobi ambapo ajenda ilikuwa kuwatimua Bw Murkomen na Bi Kihika. Maseneta hao Millicent Omanga, Iman Falhada Dekow, Waqo Naomi Jillo, Prengei Victor na Mary Seneta wanakabiliwa na hatari ya kupokonywa nyadhifa zao kwa kumkaidi Rais.

Duru katika chama hicho zinasema kwamba, Rais Kenyatta anaelekeza shoka lake kwa viongozi waliochaguliwa katika ngome yake ya Mlima Kenya, hasa wabunge, magavana na maseneta ambao wamekuwa wakimkaidi na kumdharau.

Miongoni mwa wabunge ambao wameonekana kuwa mstari wa mbele kumkaidi Rais ni Moses Kuria (Gatundu Kusini), Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira), Alice Wahome (Kandara), Purity Ngirici (Mwakilishi wa Wanawake Kirinyaga), Mithika Linturi (Seneta, Meru) na Kimani Ichung’wah (Kikuyu).

Mnamo Jumatano, katibu mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Raphael Tuju alinukuliwa akisema kwamba, chama hicho kitatangaza majina ya wabunge kinachotaka wapiga kura wawatimue.

“Hivi karibuni tutatoa majina yao. Wale ambao wamekuwa wakimdharau na kumtusi Rais ni miongoni mwa wanaolengwa. Mambo yamebadilika,” Bw Tuju alisema.

Rais Kenyatta ambaye amekuwa akionya viongozi kutoka Mlima Kenya wakome kumtusi, anatarajiwa kuongoza kampeni ya kuhimiza wapigakura kuwatimua.

Hata hivyo, ingawa Katiba inaruhusu wapigakura kuwafuta wabunge, mchakato huo ni mrefu na haujawahi kufanyika tangu Katiba mpya ipitishwe 2010. Vyama vya kisiasa pia vimeshindwa kuwatimua waasi.

Kulingana na sehemu ya 45 na 46 ya sheria ya uchaguzi, mtu au watu wakitaka kumtimua mbunge, ni lazima waungwe mkono na asilimia 30 ya wapigakura waliosajiliwa katika eneobunge analowakilisha wakiwemo asilimia 15 ya wapigakura wa kila wadi katika eneo hilo.

Alhamisi, mmoja wa wanaoegemea kundi la ‘Tangatanga’ alisema ana habari kwamba analengwa kwa sababu ya msimamo wake wa kisiasa.

“Sio siri kwamba tumekasirisha watu kwa misimamo yetu na wanatulenga kwa kila mbinu. Ninachojua ni kwamba, demokrasia katika chama chetu imefifia na tutakabiliana na kila hali,” alisema mbunge huyo aliyeomba tusitaje jina lake.

Duru zetu ndani ya Jubilee zilituarifu kuwa, Rais Kenyatta anataka kuwaonyesha makali yake.

Kulingana na Bw Tuju, chama cha Jubilee kitafuata sheria kuwaadhibu waasi.

Wabunge wanaotimuliwa na vyama vya kisiasa wamekuwa wakikimbia kortini na kupata afueni.

Wakati huo huo, wabunge wanawake, wanachama wa vuguvugu la ‘Inua Mama Jenga Jamii’, sasa wanawataka maseneta watano maalumu walioagizwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama cha Jubilee kukaidi agizo hilo.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome wandani hawa wa Naibu Rais William Ruto, wamewataka maseneta hao kuelekea kortini wakisema hawatapata haki mbele ya kamati hiyo.

“Tunawataka wenzetu walioandikiwa barua na Tuju (Raphael) wasijipeleke kwa kamati hii ambayo ni ‘mahakama bandia’ kwani hawatapata haki. Waende kortini kwa sababu tayari hatima yao imeamuliwa,” Bi Wahome aliwaambia wanahabari katika majengo ya bunge huku akiandamana na wenzake 11.

Bi Wahome alitoa mfano wa mwenzao wa Kilifi, Bi Aisha Jumwa, ambaye alikuwepo Alhamisi, aliokolewa na mahakama baada ya kufurushwa na ODM mwaka 2019.