• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
COVID-19: Mara hii hakuna mikusanyiko sherehe za Eid al-Fitr

COVID-19: Mara hii hakuna mikusanyiko sherehe za Eid al-Fitr

Na MISHI GONGO

BAADA ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan waumini wa dini ya Kiislamu hufanikisha kukamilika kwa mwezi huo kwa kusherehekea sikukuu ya ‘Idd ul-Fitr’ ambayo pia huitwa ‘Eid al-Fitr’.

Ni mazoea kwa waumini kutumia siku hiyo kutembelea familia na marafiki, kwenda katika bustani, fuo za bahari na sehemu nyinginezo zenye mandhari mazuri ya kutabaradi na kufurahia kwa pamoja.

Hata hivyo, mwaka huu mambo yatakuwa tofauti, waumini watalazimika kuadhimisha sherehe hizo majumbani mwao kufuatia janga la corona.

Zikiwa zimesalia siku chache tu kufikia sikukuu hiyo, serikali imetangaza kuendelea kwa kafyu na marufuku yaliyowekwa hasa kuingia na kutoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale kufuatia idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kusalia ya juu.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza Jumamosi kuwa marufuku yaliyowekwa – zuio na kafyu – yataendelea hadi Juni 6, 2020.

Miongoni mwa marufuku ni kutokongamana, jambo ambalo huwa maarufu siku ya Iddi.

Waumini hukusanyika katika mikahawa, baharini na bustani nzuri ambapo watoto hupelekwa kujivinjari.

Sehemu nyingine maarufu ambazo wakazi wa Pwani huzuru ni fuo za bahari, lakini tangu kutangazwa kisa cha kwanza cha corona nchini, Kaunti ya Mombasa iliamrisha kufungwa kwa fuo za bahari hadi pale virusi vya corona vitakapoangamizwa au kudhibitiwa vilivyo.

Mkazi wa mji wa Mombasa Bi Mariam Ali anasema Covid-19 ni janga ambalo limebadilisha hali ya maisha pakubwa.

“Imekuwa changamoto kubwa kwetu kuanzia mwanzo wa Ramadhan hadi sasa; misikiti ilifungwa hivyo wengi wetu tulilazimika kufanya ibada nyumbani na kusikiliza mafundisho kupitia vyombo vya habari. Kufungwa kwa soko la Marikiti na Eastleigh jijini Nairobi pia kulituzuia kununulia watoto wetu nguo za kuadhimisha sikukuu ya Iddi,” akasema.

Anasema kuwa japo inasikitisha lakini watalazimika kusherehekea majumbani mwao ili kujikinga na maambukizi.

Mombasa ni kaunti ya pili nchini inayoongoza kwa idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili, Bi Hamira Saidi anasema waumini watalazimika kutoshiriki katika ada nyingi za siku hiyo muhimu kama njia ya kulinda afya zao.

Bi Saidi anawashauri waumini kutumia teknolojia kusalimia jamii zao.

“Familia zinaweza kuzungumza kupitia video kwa simu na wale wanaoishi pamoja wanaweza kufanya shughuli kwa pamoja ili kusherehekea. Inaweza kuwa kutazama filamu nzuri pamoja au kuketi na kuzungumza,” akasema.

You can share this post!

KPL kuamua hatima ya ligi wiki hii

Magufuli amfuta kazi naibu waziri wa afya

adminleo