• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Mudavadi afanye kazi na Uhuru?

Mudavadi afanye kazi na Uhuru?

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Amani National Congress (ANC) Jumanne kitafanya mkutano wa kundi la wabunge na maseneta wake (PG) huku duru zikisema kinapanga kubuni ushirikiano na chama cha Jubilee.

Katibu Mkuu wa chama hicho, kinachoongozwa na Musalia Mudavadi, Barack Muluka amethibitisha Jumapili uwepo wa mkutano huo lakini akapuuzilia mbali uwezekano wa kujadiliwa kwa suala hilo la muungano.

“Ni kweli chama kimeitisha mkutano wa wajumbe wetu katika bunge la kitaifa na seneti kujadili masuala yetu ya ndani. Suala la kubuni muungano na Jubilee sio mojawapo ya ajenda zetu,” akasema kwenye mahojiano kwa simu.

Naye Mbunge wa Lugari Ayub Savula ambaye ndiye mwenyekiti wa kundi la wabunge wa ANC amesema mkutano huo utajadili shughuli za bunge kwa misingi ya mabadiliko ambayo Jubilee ilifanya juzi kwa uongozi wake katika seneti na mengine yanayonukia katika bunge la kitaifa.

“Mkutano wetu wa Jumanne unalenga kuweka mikakati yetu ya kufanya kazi na uongozi mpya wa chama cha Jubilee katika mabunge yote mawili. Tunaunga mkono mabadiliko hayo mradi yatawezesha mabunge hayo kuendelea kutekeleza wajibu wa kuchunguza utendakezi wa serikali kuu,” akasema Bw Savula ambaye pia ni naibu kiongozi wa ANC.

“ANC haina mipango yoyote ya kubuni muungano na Jubilee wakati huu, lakini sisi kama wabunge tutaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa wajibu wetu bungeni bila kuyumbishwa kwa njia yoyote,” akaongeza.

Bw Mudavadi ameunga mkono mabadiliko ya uongozi wa Jubilee katika Seneti yaliyofanyika katika mkutano ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi, Jumatatu juma lililopita.

“Nidhamu sharti idumishwe katika chama ili iweze kuendeleza ajenda zake bila pingamizi zozote. Kwa hivyo kiongozi wa Jubilee alikuwa na haki ya kuwaondoa wale ambao alihisi wanahujumu msimamo wa chama chake katika Seneti,” Bw Mudavadi alinukuliwa akisema Jumanne wiki jana.

Katika mabadiliko hayo, Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alipokonywa wadhifa wa kiongozi wa wengi na ukapewa Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio.

Naye Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata alitunukiwa cheo cha kiranja wa wengi baada ya mwenzke wa Nakuru Susan Kihika alitimuliwa.

Duru zinasema huenda ANC kinapania kuimarisha uhusiano wake na Jubilee ili kipewe cheo cha kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa endapo Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali atapigwa kalamu.

ANC ina wabunge 11 waliochaguliwa katika bunge la kitaifa na mbunge mmoja maalum ambaye ni Godfrey Osotsi. Na inawakilishwa na wajumbe wawili katika seneti ambao ni George Khaniri (Vihiga) na Seneta Maalum Petronila Were.

You can share this post!

Corona ilikuja wakati nikijivunia fomu ya kutisha, asema...

COVID-19: Kenya sasa ina visa 887

adminleo