Habari

Kagwe awapongeza Wakenya kwa kutilia maanani taratibu na sheria za kudhibiti Covid-19

May 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

KENYA inaendelea kukabili janga hatari la Covid-19 na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe sasa anawapongeza Wakenya akisema wanajaribu wawezavyo kufuata taratibu na sheria zilizotolewa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Akihutubu katika kikao kilichohudhuriwa na baadhi ya mawaziri kilichoandaliwa Afya House, Nairobi, Jumanne, wakati pia akitoa takwimu za maambukizi ya Covid-19 Bw Kagwe amepongeza jitihada za Wakenya kwa ushirikiano walioonyesha kudhibiti ugonjwa huo.

“Hatujashinda vita dhidi ya ugonjwa huu, lakini ni furaha Wakenya wanashirikiana na serikali kuudhibiti,” waziri amesema.

Ametoa mfano jinsi Wakenya wanavyoendesha shughuli zao za kimsingi maeneo ya mijini.

“Miezi mitatu iliyopita, Kenya iliporipoti kisa cha kwanza cha Covid-19 ambapo watu mijini hawakuwa wakivalia barakoa. Hivi sasa kila mmoja anavalia barakoa,” akapongeza.

Uvaliaji barakoa hasa katika maeneo ya umma, kunawa mikono kila mara na kudumisha umbali wa mita moja na zaidi baina ya mtu na mwenzake, ni miongoni mwa taratibu na sheria zilizotolewa na wizara kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Waziri Kagwe amehimiza Wakenya kuendelea kujikinga kuambukizwa Covid-19 kwa kuzingatia kanuni.

“Hivi si vita vya serikali pekee, ni vita vyetu sisi sote. Tumeona mtu mmoja anaweza kuambukiza watu wengi sana. Tunasihi watu wajikinge kwa kuzingatia masharti sisi Wizara ya Afya tumetoa. Nyumba au gari haliwezi ambukiza mtu Covid-19, watu ndio wanaambukizana. Tafadhali tukijinge, na tujijali sisi wenyewe,” akafafanua.

Kufikia Jumanne jioni, Kenya imekuwa na visa vipya 51 idadi jumla ya wagonjwa wa Covid-19 waliothibitishwa nchini ikigonga 963.