Habari Mseto

Mama ajifungua katika kambi alikotafuta hifadhi mafuriko yakiendelea Garissa

May 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

MWANAMKE mmoja amejifungua katika kambi alikotafuta hifadhi Kaunti ya Garissa baada ya kupoteza makazi yake kufuatia mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa katika kaunti hiyo.

Bi Shamim Hadya ni miongoni mwa wenyeji waliolazimika kuhamia kambi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani baada ya kupoteza makazi yao na mifugo kufuatia Mto Tana kuvunja kingo zake.

Alisema kwa sasa anahofia afya yake na mtoto kwani eneo hilo halina maji safi ya kunywa na vyoo.

“Eneo hili si salama kwetu kuishi kufuatia hali duni ya mazingira,” akasema Bi Hadya.

Alielezea kuwa hema ambalo ndilo limekuwa hifadhi ya kuwasitiri, ni dogo na hali huwa mbaya zaidi jua linapowaka.

“Watu wameweka mahema yao karibu. Hatuna nafasi ya kutosha. Hali zetu za afya iwapo kutatokea kisa cha virusi vya corona itakuwa hata mbaya zaidi kwa sababu ya msongamano kambini, ”akasema Bi Hadya.

Alisema yeye hana chakula cha kutosha kuilisha familia yake.

“Tunaomba serikali ya kaunti itukumbuke na sisi. Ukosefu wa chakula ndio changamoto yetu kuu. Tunaishi kama hatuko katika nchi yetu wenyewe,” akasema Bi Hadya.

Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu zaidi ya familia 700 zilipoteza makazi yao kutokana na mafuriko.

Haya yanajiri huku watu 7,000 katika Kaunti ya Mandera wakilazimika kulala nje baada ya Mto Dawa kuvunja kingo zake.

Gavana wa Kaunti hiyo Ali Roba alieleza kuwa kuna uwezekano kwa kaunti hiyo kukumbwa na baa la njaa kufuatia mazao kusombwa na mafuriko.

“Tumeweka mikakati kluhakikisha kuwa vyakula na bidhaa zingine muhimu zinagawanywa kwa sehemu zilizoathirika na mafuriko hayo,” akasema gavana Roba.