Aporwa mchana peupe mara baada ya kushuka kutoka kwa matatu Githurai
Na SAMMY WAWERU
VISA vya uhalifu katika mtaa wa Githurai vimeanza kufufuka, wakazi wakilalamikia kuporwa mchana peupe na wezi.
Alhamisi katika kituo cha matatu zinazohudumu baina ya mtaa huo na jiji la Nairobi, mwanamume mmoja amelalama akisema amenyang’anywa na kundi la vijana aliodai walikuwa wakishawishi abiria kuingia kwenye matatu.
“Wameniibia simu na pesa baada ya kushuka kwenye basi,” akalalama, akifichua kwamba alinyang’anywa simu yenye thamani ya Sh6,000 na Sh2,000 pesa taslimu.
Kulingana na walioshuhudia na kumuokoa mwanamume huyo aliyepigwa na kuporwa mchana hadharani, hicho si kisa cha kwanza kuonekana hasa tangu janga la Covid-19 kuripotiwa nchini.
“Wizi wa simu, watu kuporwa pesa na bidhaa wanazobeba, ni uhalifu ambao umeanza kufufuka katika mtaa wa Githurai,” amesema mkazi aliyekuwa katika eneo la mkasa.
Mwathiriwa ni fundi wa pasi na waliomuokoa walifanikiwa kunusuru mojawapo ya kifaa hicho.
Tukio hilo limejiri siku mbili baada ya mshukiwa wa wizi wa simu katika kituo hicho cha matatu kunusurika kifo.
Visa vya uhalifu vinaendelea kushuhudiwa, licha ya kituo cha polisi cha Githurai kuwa chini ya umbali wa kilomita moja kutoka eneo hilo.