Michezo

Sofapaka wataka AFC Leopards waombe msamaha kwa kuwadunisha

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Sofapaka kinachoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) sasa kinataka mwenyekiti wa AFC Leopards, Dan Shikanda, awaombe msamaha.

Mnamo Jumamosi ya Mei 23, 2020, Shikanda aliyekuwa akihojiwa na mojawapo ya mashirika ya habari ya humu nchini, alisema kwamba hakuna soka yoyote humu nchini bila Gor Mahia na AFC Leopards.

Kauli hiyo haikupokelewa vyema na Rais wa Sofapaka, Elly Kalekwa.

Katika mahojiano hayo, Shikanda alizidi kueleza kuwa alifahamu KCB kuwa benki wala si timu ya soka na kwamba aliwahi kusikia pia kuwepo kwa kikosi kilichojiita Sofapaka katika kipute cha KPL.

Katika taarifa kwenye mtandao rasmi wa kijamii wa Sofapaka, Kalekwa alishikilia kwamba kauli za Shikanda kuhusu vikosi vingine vya KPL, hususan Sofapaka, zilikosa kuzingatia heshima na akamtaka kuomba msamaha.

Kalekwa ambaye ni mzawa wa Congo, alisema Sofapaka wanastahiki heshima hasa ikizingatiwa ukubwa wa mafanikio yao katika soka ya bara Afrika na Ligi Kuu ya KPL walioanza kuinogesha mnamo 2009.

Aidha, alisisitiza kwamba vikosi vyote vya KPL vinastahili kuzungumziwa kwa hadhi hasa ikizingatiwa kwamba Leopards waliwahi kuteremshwa daraja kwenye kipute cha KPL mnamo 2008.