Sanchez ana risasi moja pekee ya kujiokoa Inter Milan
Na CHRIS ADUNGO
INTER Milan wamethibitisha kwamba fowadi Alexis Sanchez atasalia nao hadi mwisho wa msimu huu akisubiri iwapo usimamizi wa kikosi hicho utampa mkataba wa kudumu au la.
Hii ni baada ya Manchester United ambao ni waajiri wa mfumaji huyo wa zamani wa Barcelona na Arsenal kushikilia kwamba hawamhitaji tena Sanchez ugani Old Trafford.
Soka ya Italia msimu huu ilicheleweshwa na janga la corona ambalo vinginevyo lingempa Sanchez ambaye ni mzawa wa Chile fursa ya kubanduka ugani San Siro mwezi huu.
Kwa mujibu wa Piero Ausillo ambaye ni mkurugenzi wa michezo wa Inter, Sanchez atapata nafasi kadhaa za kudhihirishia usimamizi uwezo wake ugani kwa mara ya mwisho kabla ya mustakabali wake kuamuliwa.
Sanchez anayechezea Inter kwa mkopo kutoka Man-United, hata hivyo amefichua maazimio ya kurejea Chile na kujiunga na kikosi chochote cha Ligi Kuu ya taifa hilo kabla ya kustaafu soka.
Kipute cha Serie A kinatarajiwa kuanza upya mnamo Juni 20 baada ya Waziri wa Micheo, Vincenzo Spadafora kuthibitisha hilo.
Majeraha ya mara kwa mara yamelemaza kabisa makali ya Sanchez ambaye anajivunia bao moja pekee kutokana na mechi 15 zilizopita ndani ya jezi za Inter.
Sanchez amewajibishwa na Chile katika jumla ya mechi 132 na kupachika wavuni mabao 43. Ushawishi wake ugani ulikuwa mkubwa katika fainali tatu zilizopita za kombe la Copa America.
Man-United wanafikiria pia uwezekano wa kumtuma Sanchez hadi Borussia Dortmund kwa matarajio kwamba hatua hiyo itawafanya miamba hao wa soka ya Ujerumani kuwa wepesi wa kuwapatia chipukizi Jadon Sancho.