• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Afueni kwa wakulima ujenzi wa kiwanda cha unga ukikamilika

Afueni kwa wakulima ujenzi wa kiwanda cha unga ukikamilika

ONYANGO K’ONYANGO na BARNABAS BII

WAKULIMA wa mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wanatarajiwa kupata afueni kufuatia kukamilishwa kwa ujenzi wa kiwanda cha kusaga unga wa mahindi.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Moi-Soy, Belfast Sang, jana alisema kuwa kiwanda hicho kimejengwa kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu kwa kima cha Sh477 milioni.

Alisema kuwa sababu ya kujenga kiwanda chao ni kujikinga dhidi ya kupunjwa na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakinunua mahindi yao kwa bei duni.

“Nimewasihi wanachama wa Chama cha Ushirika cha Moi-Soy kwamba kuongeza mashamba yao ya kukuza mahindi. Hii ni kwa sababu kiwanda chao ambacho kitaanza kufanya kazi mwishoni mwa mwaka huu, kitahitaji mahindi ya kutosha,” akasema Bw Sang.

Kulingana na waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara wa Kaunti ya Nandi Esther Mutai, serikali ya kaunti imechangia Sh230 milioni katika ujenzi wa mradi huo. Wanachama wa chama hicho cha ushirika walichangia jumla ya Sh247 milioni.

“Serikali imetoa Sh230 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho. Lakini fedha hizo zimetolewa kama mkopo kwa chama cha ushirika. Shughuli ya kuweka mashine itakamilika Oktoba na usagaji wa unga wa mahindi utaanza Desemba,” akasema Bi Mutai.? “Wakulima wanamiliki kiwanda hicho kupitia chama chao cha ushirika na sasa watashindana na viwanda vinginevyo vya unga wa mahindi,” akaongezea.

Serikali ya kaunti inaamini kuwa kiwanda hicho kitakinga wakulima dhidi ya ushindani mkali ambao husababishwa na mahindi yanayofurika humu nchini kutoka katika mataifa jirani.? “Mahindi kutoka mataifa jirani kama vile Uganda huharibia soko wakulima wa humu nchini. Serikali ya Kaunti sasa itakuwa inaagiza mahindi kutoka mataifa jirani kupitia kiwanda hicho. Kwa kufanya hivyo, bei ya mahindi itasalia thabiti kwani tutaagiza tu mahindi ya kukabiliana na uhaba uliopo,” akasema.

Serikali ya kaunti ilisema kuwa mradi huo utanufaisha wakulima wote kutoka katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa ambalo huzalisha chakula kinachotumiwa katika maeneo mengi ya nchi.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wameonya kuwa Kenya huenda ikakumbwa na uhaba wa chakula katika siku za usoni kufuatia hatua ya wakulima kupunguza mashamba ya kukuza mahindi.

Wakulima wamekuwa wakilalamikia kufurika kwa mahindi kutoka Uganda huku wakisema kuwa yamewafanya kupata hasara kubwa.

You can share this post!

Mwili wa mvulana aliyeuawa na mamba wapatikana

Ndani kwa kubaka msichana usiku mzima

adminleo