MAHANGAIKO: Baadhi ya wakazi wa Mayungu wategemea dampo kupata chakula
Na FARHIYA HUSSEIN
TUNAKARIBISHWA na taka zilizooza na kuozeana na kutapaka kila mahali huku zikitoa uvundo eneo la Mayungu, Malindi, Kaunti ya Kilifi.
Tunampata Bi Kadzo Kenga akichakura taka hizo.
Anasema anatafuta chakula. Eti haya ndiyo mazoea.
Kila siku hapa Mayungu, yeye hujiunga na wakazi wengine kutafuta chakula kutoka kwa mabaki yaliyoshushwa na lori la takataka.
Wengi hawawezi kuvumilia harufu hiyo kali wala kuishi sehemu kama hii, lakini kwao, hapa ni kama mgodi wa kujichumia riziki.
“Mume wangu mlemavu alichukuliwa na watu wa familia yao na wakaniacha hapa na watoto sita ambao ninawalea. Tumezoea maisha haya kwani hakuna kazi inayopatikana karibu na eneo hili,” anasema Bi Kenga ambaye ni mjamzito.
Taifa Leo imebaini kuwa mara tu lori linakaribia eneo hilo, nyuso za wakazi zinajawa na furaha.
“Tunakula kila aina ya chakula kuanzia ngano, slesi za mkate na wali. Yaani kimsingi hakuna kilichooza kwetu. Ikiwa tutapata chakula hicho, tunayo bahati kwa sababu nyakati zingine tunalazimika kulala njaa,” anaeleza Bi Kenga.
Karibu na nyumba yake, kuna mwanamke mwingine anayeonekana akiwalisha wanawe.
“Hatuwezi kununua chakula kwa hivyo badala yake tunategemea lori linaloleta makombo kwenye dampo,” anasema mwanamke huyo anayejitambulisha kwamba anaitwa Bi Rehema Wanje.
Si wanawake tu. Nalo lipo kundi la wanaume wanaonekana wakichakura nao wapate cha kutia kinywani kiingie tumboni na kingine wapeleke nyumbani.
Mwanamume kwa jina Bw Hamisi Changawa anasema amekosa njia nyinginezo halali za kujitafutia riziki.
“Tumelazimika kutafuta chakula hapa,” anasema.
Mkazi mwingine wa Mayungu, Bw Ngumbao Elvis anakubaliana na alichokisema Bw Changawa.
“Ndio; tunaugua kwa kula hivi vyakula, lakini ni kipi tunastahili kufanya? Tusibiri miujiza?”anauliza mkazi huyo.
Watoto nao pia hawajaachwa nyuma kwani nao wanahangaika papa hapa wakichukulia hali hii kuwa ya kawaida.
Mtoto mwenye umri wa miaka 12 anasema huamka asubuhi na mapema na hatua yake inayofuata ni kufika dampo kuona ikiwa lori la taka lilikuja na kuacha mabaki yoyote au la.
“Mimi ni mtoto wa pili katika familia ya watoto watano. Nimezaliwa na kukuzwa hapa. Hii imekuwa njia yetu ya kulelewa, kuamka na kwenda kutafuta chakula katika dampo,” kijana huyo alisema. Taifa Leo haiwezi kumtaja jina kwani yeye ni wa umri mdogo.