Habari Mseto

NZIGE NA MAFURIKO: Wakulima Garissa kufadhiliwa na serikali ya kitaifa na ya kaunti

June 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

ZAIDI ya wakulima 30 katika Kaunti ya Garissa watafaidika wakisubiri kufadhiliwa na Serikali ya Kitaifa na Kaunti kupitia Programu ya Msaada wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo.

Waliathirika zaidi kutokana na uvamizi wa nzige na mafuriko.

Waziri wa Kilimo, Mifugo, na Ushirika kaunti hiyo, Bw Mohamed Shale ambaye Jumanne alifungua rasmi mkutano wa Jukwaa la Tathmini ya Ukwasi wa Kaunti ya Garissa katika hoteli ya Garissa, alisema mpango wa ufadhili utasaidia sana wakulima kwani imefika wakati unaofaa.

“Programu ya ASDSP11 itasaidia kikundi cha wakulima 30 katika kila mwaka wa fedha ili kuongeza tija ya mkulima,” alisema.

Wakulima ambao huvuna nyanya, nyama ya ng’ombe na maziwa ya ngamia walihimizwa kuja na maoni halali kabla ya Agosti kwa idhini.

“Wakulima wa mazao waliathirika na mafuriko na uvamizi wa nzige na wakapoteza mali nyingi. Kuna uwezekano wa wimbi la pili la uvamizi wa nzige tena kwa fujo kutoka Yemen kupitia Somalia jinsi ilivyoonya FAO na wataalam wengine ambao walikuwa wakifuatilia mwenendo wa uvamizi wa nzige,” akasema Bw Shale.

Alisema serikali ya kaunti imejiandaa kikamilifu kutoa msaada wa vifaa na tayari mafunzo yanaendelea kwa wafanyakazi wanaopambana na janga la nzige.

Alitoa wito kwa wakulima kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Mratibu wa Programu ya Msaada wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Garissa Dkt Ahmed Hassan alisema mafunzo zaidi kwa wahusika wa uzalishaji mali yataendeshwa kwa miongozo ya utaratibu wa ruzuku, muundo wa pendekezo la uvumbuzi na kumbukumbu ya ufahamu.