COVID-19: Serikali kuu na zile za kaunti zakubaliana kushirikiana katika ufunguzi wa sekta mbalimbali
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI Kuu na Serikali 47 za kaunti zimekubaliana kuwahusisha magavana katika mipango yote ya kufungua uchumi, majumba ya ibada na shule.
Katika mkutano ulioshirikisha magavana na ambao ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi Jumatano, chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, magavana walikubaliana na wazo la Rais Uhuru Kenyatta kwamba kila kaunti iwe na vitanda 300 vya kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19 ifikapo Julai 6.
“Hatua hiyo inalenga kulinda maisha ya Wakenya dhidi ya madhara ya kiafya na kiuchumi yanayotokana na Covid-19,” ikasema taarifa kutoka kitengo cha habari za Rais.
Kando na kuongeza idadi ya vitanda katika vituo maalum vya kuwahudumia waathiriwa wa ugonjwa huo, serikali za kaunti pia zilitakiwa kuifanyia mabadiliko mipango ya kifedha na kimaongozi ili kujumuisha mikakati ya kupambana na Covid-19.
Mipango hiyo itaanza kutekelezwa mwaka huu 2020 hadi mwaka 2021.
Na ili kushughulikia presha kutoka kwa umma ya kutaka makanisa na misiki ifunguliwe, mkutano huo ulikubaliana kwamba Baraza la Magavana lihusishwe katika mazunguzo yanayoendelea kati ya serikali kuu na viongozi wa kidini.
“Isitoshe, ili kufanikisha mpango wa kufunguliwa kwa shule na taasisi zingine za elimu ya juu, imekubaliwa kuwa magavana wahusishwe katika mazungumzo yanayoendelea kati ya wadau,” taarifa hiyo ikaongeza.
Mazungumzo hayo yanayoendelea chini ya uongozi wa Waziri wa Elimu George Magoha yanalenga kuchangia kutolewa kwa kalenda mpya ya shule. Hii ni kulingana na amri iliyotolewa na Rais Kenyatta juzi ambapo alitangaza kuwa shule zitafunguliwa Septemba japo chini ya masharti makali.
Ili kufuatilia utekelezaji wa maamuzi yalifikiwa Jumatano, washiriki katika mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, wamekubaliana kukutana tena Jumatano wiki ijayo kuchambua tena mwongozo kuhusu kufunguliwa upya kwa uchumi.
Rais Kenyatta ametoa wito kwa ngazi hizo mbili za serikali kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupata suluhu sawa kwa changamoto za kimaisha zilizosababishwa na Covid-19.
“Ni wakati kama huu wa shida ambapo ngazi mbili zinahitaji kuketi na kuibua suluhisho kwa majanga kama vile Covid-19,” ameeleza.
Rais Kenyatta ameongeza kuwa huu ndio wakati mwafaka ambapo taifa hili linapasa kuimarisha huduma za afya kote nchini.
“Hili janga pia ni baraka kwa upande mwingine. Limetuzindua na kutochochea kuongeza ari ya kuimarisha sekta yetu ya afya kuanzia ngazi ya kitaifa hadi mashinani. Tunapasa kulipa kipaumbele haja ya kuhakikisha kuwa hospitali zetu zina vifaa na wahudumu tosha wa afya,” akaeleza.
Wagavana wote 47, wakiongozwa na mwenyekiti wao Wycliffe Oparanya, wamehudhuria mkutano huo.
Wengine waliohudhuria ni Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na Mkurugenzi wa Afya Dkt Patrick Amoth.