Daraja lasombwa na maji ya mafuriko Nyandarua
Na SAMMY WAWERU
WENYE magari, madereva wa matatu na watumizi wengine wa barabara kati ya Njabini na Olkalou wametakiwa kutafuta njia mbadala baada ya daraja linalounganisha maeneo hayo mawili kusombwa na maji ya mafuriko Jumatano.
Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu, daraja la Thitai katika barabara ya Njabini-Olkalou liliporomoka baada ya Mto Malewa kuvunja kingo zake kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa Nyandarua.
“Shughuli za uchukuzi Njabini-Olkalou zimetatizika baada ya Mto Malewa kuvunja kingo zake na kusomba daraja Thitai lililo kati ya Kariuamu na Olkalou Mjini, Nyandarua,” Shirika hilo limeeleza katika taarifa.
Likashauri: “Watumizi wa barabara hiyo wawe waangalifu na watumie njia mbadala.”
Tangia mapema wiki hii, maendeleo mbalimbali nchini yameendelea kupokea mvua kubwa.
Baina ya miezi ya Machi hadi Mei, kumeshuhudiwa kiwango kikubwa cha mvua maeneo mengi nchini.
Tayari zaidi ya watu 280 wameaga dunia kutokana na athari hasi za mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Maelfu waliachwa bila makao, baada ya makazi yao na mali kusombwa na maji. Wakulima walikadiria hasara isiyomithilika kufuatia mimea, mazao na mifugo, kusombwa na mafuriko.
Wanaoishi pembezoni mwa mito na pia mabwawa, wanashauriwa kuhama mara moja ili kukwepa hatari inayowakodolea macho ya kusombwa na maji, mito na mabwawa inapofurika na kuvunja kingo zake.