Mto Tana wavunja maisha ya wakazi 3,000
NA KLUME KAZUNGU
WAKAZI wapatao 3000 wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na maji kwenye vijiji vya Chalaluma, Dide Waride, Moa na Matabore, Kaunti ya Lamu.
Hii ni kufuatia kuvunjika kwa kingo za mto Tana na ule wa Nyongoro, hivyo kupelekea maji ya mafuriko kutapakaa kwenye vijiji vilivyoko karibu.
Akithibitisha hayo Jumapili, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono, alisema familia 287 kutoka vijiji vya Chalaluma na Dide Waride zimelazimika kutafuta makao sehemu nyingine baada ya nyumba zao kubebwa na maji.
Alisema familia nyingine 82 zimekosa pa kuishi baada ya nyumba zao kubomolewa na maji ya mafuriko eneo la Moa.
Kijijini Matabore, zaidi ya mifugo 1000 wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo wako kwenye hatari ya kuangamia baada ya kijiji hicho kuzingirwa na maji yaliyotapakaa kutokana na kuvunjika kwa kingo za mto Tana zaidi ya siku nne zilizopita
Bw Rono alisema kufikia jana, timu ya maafisa wanaowakilisha serikali kuu eneo la Lamu kwa ushirikiano na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu tayari walikuwa wamefika kwenye vijiji husika ili kutathmini hali na kuwasaidia.
“Hali zi nzuri kwa sasa. Nyumba kadhaa zimesombwa na maji Chalaluma, Dide Waride na Moa. Tuko na zaidi ya watu 3000 ambao wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko. Tumetuma timu maalum kwenye vijiji husika ili kuwapa chakula na misaada mingine. Pia tutapeleka misaada zaidi kufikia Jumanne,” akasema Bw Rono.
Kwa upande wake, Chifu wa Dide Waride, Abdi Bocha alieleza hofu ya kuzuka kwa maradhi yanayochangiwa na maji chafu hasa kwenye vijiji vyote viliovypoathiriwa na mafuriko hayo.
Bw Bocha alisema baa la njaa pia huenda likakumba vijiji husika kwani barabara zinazotumiwa na wakazi kufikia maduka zimeharibiwa na mafuriko hayo.
“Barabara ya Chalaluma kwenda Moa imevunjika na haipitiki kwa sasa. Ukitaka kufika maeneo hayo lazima utumie boti au ndege. Maji chafu yamezingira nyumba nyingi na hii huenda ikachangia mkurupuko wa maradhi.
Tungeomba wahisani kufikisha misaada, ikiwemo vyakula, malazi, vyandarua vya kukinga wakazi dhidi ya mbu na pia dawa,” akasema Bw Bocha.
Naye Mwenyekiti wa Vijana eneo hilo, Bwanamkuu Fumo, aliomba serikali kuu, mashirika yasiyo ya kiserikali na wahisani kujitokeza ili kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko hayo ambao wengi wao ni kutoka jamii za wafugaji wa kuhamahama na wavuvi.