Kanuni kali kudumishwa ferini hata baada ya virusi
Na MISHI GONGO
SERIKALI inapanga kudumisha kanuni kali zinazotekelezwa katika kivukio cha feri Likoni, Kaunti ya Mombasa, zitadumishwa hata baada ya janga la corona kudhibitiwa kikamilifu.
Kulingana na mratibu wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata, msongamano na vurugu katika kivuko hicho vimekuwa vikisababisha uhalifu ikiwemo wanawake kunajisiwa, na abiria kuporwa.
Akizungumza na Taifa afisini mwake, Bw Elungata alisema hatua ya kuwaagiza abiria kuwekeana umbali wa mita moja imesaidia kupunguza uhalifu.
“Tutahakikisha kuwa maafisa wa usalama watasalia katika kivuko hicho kuhakikisha kuwa abiria wanatekeleza masharti yaliyopo,” akasema.
Kila siku kivuko cha feri hutumiwa na takriban watu 300,000 na magari 6,000.
Bi Rehema Mzee, mkazi wa Likoni anayetumia kivuko hicho kila siku, alisema kwa sasa anafurahia huduma za shirika hilo kufuatia utulivu unaoshuhudiwa.
“Tulikuwa tunashuhudia wazee kwa watoto wakikanyagwa katika vurumai ambazo huzuka saa za jioni na alfajiri watu wanapokimbilia vibaruani lakini kwa sasa hali ni shwari,” akasema.
Mkazi mwengine Bi Irene Mwangi ambaye ni muuzaji bidhaa katika eneo la Shonda, Likoni, alisema awali walipoteza mizigo yao kwa wabebaji ambao walitoweka nayo katikati ya halaiki kubwa ya watu.
“Wahudumu wengi wa vibanda hutoa bidhaa zao soko la Kongowea, tukifika katika kivuko hichi huwapa wabebaji ili kutusaidia. Baadhi yao hujiingiza katika makundi ya watu na kutoweka, lakini tangu kuwekwa sheria mpya hilo haliwezekani,” akasema.
Manufaa mengine ambayo yanashuhudiwa Pwani kwa kanuni za kudhibiti corona ni uhifadhi wa fuo na bahari.
Katika mahojiano ya awali, wataalamu wa mazingira walisema tangu kuwekwa kwa kafyu mazingira yamekuwa safi.
Kabla kufungwa kwa fuo za bahari, maelfu ya wakazi walikongamana katika fuo za bahari katika eneo la Pwani kujivinjari. Hali hiyo ilisababisha uchafuzi kwa utupaji taka kiholela.
Aidha marufuku ya kukongamana yamesitisha disko matanga na disko vumbi katika Kaunti ya Kilifi ambaya yalikuwa yanasababisha mimba za mapema miongoni mwa vijana.
Kulingana na Kamishna wa polisi katika eneo hilo Magu Mutindika, jam visa vya mimba za mapema bado vinashuhudiwa japo vimepunguwa pakubwa.
Katika sekta ya hoteli na utalii, Bw AbdulAziz Ali alisema maduka ya jumla pia yanapaswa kuendeleza kanuni za usafi baada ya janga la corona.