• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Mikakati anayohitaji Mudavadi kukabili papa na nyangumi wanaotawala bahari ya siasa

Mikakati anayohitaji Mudavadi kukabili papa na nyangumi wanaotawala bahari ya siasa

Na WANDERI KAMAU

HUKU wanasiasa wakiendelea kusuka karata kuhusu mbinu watakazotumia kuibuka washindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, miongoni mwa wale wanaotazamwa kwa karibu ni kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.

Katika siku za hivi majuzi, Bw Mudavadi amekuwa akikutana na viongozi wa siasa kutoka sehemu mbalimbali nchini, kwenye hatua ambayo wadadisi wanaitaja kuwa ishara za mapema kuwa mwanasiasa huyo anajenga muungano utakaomwezesha kufika Ikulu.

Miongoni mwa wanasiasa aliokutana nao kufikia sasa ni kiongozi wa Narc-Kenya Bi Martha Karua, waziri wa zamani Dkt Sally Kosgey, mwanasiasa Peter Kenneth na jumbe kutoka sehemu zingine nchini.

Bw Mudavadi pia ameendelea kuwa na uhusiano wa karibu na kiongozi wa Ford-Kenya, Seneta Moses Wetang’ula wa Bungoma.

Kando na hayo, amekutana na baadhi ya wabunge wa Magharibi ambao wanaegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ katika Chama cha Jubilee (JP), vyama vya ANC na Ford-Kenya.

Hata hivyo, upeo wa mikakati hiyo ni kauli iliyotolewa wiki iliyopita na Katibu Mkuu wa ANC, Bw Barack Muluka, kuwa Naibu Rais William Ruto amekubali kumuunga mkono Bw Mudavadi kwenye kinyang’anyiro hicho.

Na licha ya kauli hiyo, Dkt Ruto hajakubali wala kukanusha madai hayo, hali ambayo wadadisi wanataja kuwa ishara ya wazi wawili hao wanapanga kubuni muungano wa kisiasa ielekeapo 2022.

Hata hivyo, maswali yaliyopo ni ikiwa muungano huo utafanikisha jahazi lake kufika ikulu, ikizingatiwa kuwa baadhi ya wanasiasa hao wamejaribu kuwania nyadhifa mbalimbali au hata urais hapo awali bila mafanikio.

Kulingana na Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa, Bw Mudavadi anaonekana kuiga mfumo wa “Pentagon” uliotumiwa na ODM mnamo 2007, kwa lengo la kuwakilisha kila eneo.

Licha ya hayo, anasema kuwa lazima awashirikishe wanasiasa wenye ushawishi zaidi, kwani ufuasi wa baadhi ya wale aliowajumuisha si wa kutosha.

“Ingawa Bw Mudavadi anaonekana kuweka juhudi kujiuza kama kiongozi anayewakilisha sura ya kitaifa, lazima ajaribu kuwavutia wanasiasa wenye ushawishi katika maeneo yao, kwani ni kupitia hilo pekee atakavyoimarisha ushindani wake,” asema Bw Mutai.

Kwa mfano, anamtaja Bi Karua kuwa mwanasiasa mkakamavu na mwenye msimamo thabiti kisiasa, ila asiye na ushawishi wa kutosha katika eneo la Mlima Kenya, ikilinganishwa na wanasiasa kama Rais Uhuru Kenyatta.

KARUA NA KENNETH

Bi Karua aliwania ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga 2017 lakini akashindwa na Gavana Anne Waiguru.

Mdadisi huyo anamtaja Bw Kenneth kuwa mwanasiasa asiye na ushawishi wowote, kwani taswira yake ni ya “mwanasiasa aliyejengwa” badala ya kujijenga mwenyewe.

Vile vile, anamtaja Kenneth kuwa kiongozi ambaye mizizi yake inatiliwa shaka na wengi, hasa baada ya kuwania ugavana katika Kaunti ya Nairobi mnamo 2017.

Hii ni licha ya kuhudumu kama mbunge wa Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

“Wawili hao bila shaka si chaguo ambalo Bw Mudavadi anaweza kulitegemea, kwani walikosa kudhihirisha ushawishi wao walipowania urais mnamo 2013 na kushindwa kutwaa ugavana mnamo 2017. Ikiwa atawabaki nao, basi itamlazimu awatafute viongozi zaidi,” akasema.

Na kwa kumshirikisha Dkt Ruto, wadadisi wanalitaja hilo kama “kosa”, kwani licha ya kuwa mwanasiasa shupavu, anaandamwa na changamoto nyingi, baadhi zikiwemo juhudi za watu wenye ushawishi serikalini na Jubilee kumzima kisiasa.

Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa, anamtaja Dkt Ruto kuwa mwanasiasa ambaye nyayo zake zinafuatwa kwa ukaribu popote aelekeapo.

“Juhudi zinazoendelea katika Jubilee ni za kumzima Dkt Ruto kisiasa, ili kuhakikisha kuwa ushawishi wake umepungua. Hivyo, ingawa bado hilo halitamzima kabisa, ushawishi wake utakuwa umeshuka kwa kiasi kikubwa, ikilinganishwa na ilivyokuwa 2013 ama 2017,” akasema Bw Muga.

Hivyo, anasema kuwa itamhitaji Bw Mudavadi kupanua mkono wake kisiasa katika Bonde la Ufa kuwaleta wanasiasa zaidi ili kujaza pengo litakalokuwa limeachwa na Dkt Ruto.

Dkt Kosgey naye anatajwa kuwa mwanasiasa “asiyeingiliana na kizazi cha sasa” hasa baada ya kuhudumu kwa muda mrefu katika serikali ya marehemu Daniel Moi.

Lakini licha ya changamoto hizo, wadadisi wanasema huenda Bw Mudavadi na Dkt Ruto wakafanikiwa kuvumisha muungano huo, ikizingatiwa walikuwa pamoja kwenye kundi la “Pentagon”.

“Hawa ni wanasiasa wanaofahamu kwa undani mikakati ya kisiasa katika ODM na Jubilee. Hivyo, ni mapema kupuuzilia mbali muungano wao kwani ni dhahiri wana washauri wao ambao wanawasaidia kulainisha mikakati yao,” asema Bw Muga.

Na kwa kuwa wote “wamesalitiwa” kisiasa na Bw Raila Odinga hapo awali, wadadisi wanasema kuwa uwepo wake Bw Odinga kwenye kivumbi hicho huenda ukashinikiza umoja wao zaidi wakilenga “kulipiza kisasi” dhidi ya usaliti huo.

You can share this post!

Wanasiasa waanza harakati za kusaka mrithi wa Maraga

Mkutano wa Weta watibuliwa kwa vitoa machozi

adminleo