• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Kaunti ya Nakuru yalenga kuwa na vitanda 1,000

Kaunti ya Nakuru yalenga kuwa na vitanda 1,000

Na PHYLLIS MUSASIA

Kaunti ya Nakuru inatarajia kuongeza idadi ya vitanda katika maeneo yaliotengwa hospitalini kwa ajili wa wagonjwa wa Covid-19 hadi 1,000, kufikia mwishoni mwa Julai.

Juhudi hizi ni kufuatia maagizo ya Wizara ya Afya kwamba kila kaunti inastahili kuwa na angalau vitanda 300 vilivyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa virusi vya corona ili kusaidia katika kupambana na janga hilo.

Alipozuru ujenzi wa jengo jipya katika Hospitali ya Nakuru, Gavana Lee Kinyanjui alisema kaunti yake inajizatiti kuhakikisha kwamba imejiandaa vilivyo kupambana na janga la corona iwapo maambukizi yatazidi.

Kulingana naye, jengo hilo lenye ghorofa tatu ambalo lilikuwa limeratibiwa kuwa kitengo cha matibabu ya nje, litabatilishwa kuwa hospitali ya matibabu ya wagonjwa wa corona msimu huu.

“Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika kwa muda siku 60 zijazo. Wakati huu wahandisi wako katika kipindi cha lala salama kuhakikisha kuwa jengo hili linapata kazi msimu huu wa janga,” akasema Bw Kinyanjui.

Jengo hilo lenye thamani ya Sh500 milioni kulingana na Bw Kinyanju, litakuwa na jumla ya vitanda 500 pamoja na itengo maalumu cha utunzaji mkubwa kwa wagonjwa watakao hitaji huduma hizo.

Aliongeza kuwa idara ya afya inaendeleza mipango ya kuongeza idadi ya wauguzi na madaktari ili kuafikia malengo yake.

Jengo jipya la huduma za matibabu katika Hospitali ya Nakuru. Picha/ Phyllis Musasia

Kufuatia ongezeko la kesi za wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona nchini, Bw Kinyanjui alisema madereva wote wa magari aina ya trela ambao husafirisha mizigo kutoka amana ya mizigo eneo la Mai Mahiu kaunti ndogo ya Naivasha watahitajika kupimwa hali yao kabla ya kuruhusiwa kuingia Nakuru.

Kulingana naye, sehemu hiyo huusisha watu wengi kutoka sehemu mbalimbali swala mbalo linapaswa kushughulikiwa kwa kina msimu huu wa janga hatari.

Waziri wa Afya Dkt Kariuki Gichuki alisema kuna haja kubwa ya serikali ya Nakuru kuimarisha kanuni za kujikinga kutokana na maambukizi ya virusi vya corona kwani eneo nzima hutumika katika usafiri wa kila siku.

“Itakuwa vigumu kwetu ikiwa kaunti ya Nakuru itasambaa maambukizi kama vile tunavyoona katika kaunti za mipakani.

Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui alipozuru hospitali ya Nakuru ambapo ujenzi wa jumba la ghorofa tatu linajengwa kwa ajili ya wagonjwa walioambukizwa virusi vya Corona. Picha/Phyllis Musasia

Kulingana naye, Nakuru ina jumla ya vitanda 140 vilivyotengwa kwa wagonjwa wa virusi vya corona na ambavyo vimewekwa katika hospitali za Nakuru, Langalanga, Gilgil, Molo na Naivasha.

Aidha kunavyo vitanda kumi vya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kiwango cha juu pamoja na mashine za kupumua 40.

Nakuru imerokodi zaidi ya visa 15 vya maambukizi huku watu wanne wakitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

You can share this post!

Rakitic apiga bao la pekee Barca ikiilemea Bilbao

Serikali yakiri corona inachangia mimba za mapema

adminleo