Visa vya akina mama kulipwa miraa mabinti wakilala na wazee vyaripotiwa Lamu
Na KALUME KAZUNGU
BAADHI ya akina mama kwenye vijiji vingi vya Waboni, Kaunti ya Lamu wamelaumiwa kwa kushawishika kulipwa miraa na sukari mabinti wakilala na wazee.
Hali hiyo imesababisha wasichana wadogo wa kati ya umri wa miaka 15 na 16 kuishia kubeba ujauzito na kuolewa na wazee wa umri wa miaka 59 na zaidi.
Kisa cha hivi punde zaidi ni kile cha kijiji cha Mswakini, tarafa ya Hindi, ambapo msichana, 16, wa darasa la sita alipachikwa mimba na mzee wa umri wa miaka 59 baada ya mamake msichana huyo kulipwa miraa, muguka na kilo kadhaa za sukari.
Katika mahojiano na Taifa Leo mwishoni mwa juma, Mwenyekiti wa Maendeleo ya Akina Mama wa Jamii ya Waboni Bi Nana Abuli, alisema inasikitisha kuona kwamba akina mama wanaendelea kuwa kikwazo katika uimarishaji wa elimu ya mtoto wa kike eneo hilo.
Alisema wengi wamekosa kuwajibikia malezi ya watoto wao wasichana, hivyo kuwaruhusu kuendelea kushiriki vitendo vya ngono na wazee ilmuradi wapate bidhaa kadhaa.
Bi Abuli alieleza haja ya wahisani kujitokeza na kuzindua kampeni kabambe ya kuielimisha jamii ya Waboni kuhusu umuhimu wa elimu ya mtoto wa kike.
“Wanawake wengi hapa ni waraibu wa muguka na miraa na wako tayari kuwaruhusu wasichana wao wa shule kushiriki ngono na wazee ili nao wawalipe miraa, muguka na sukari,” akasema Bi Abuli.
Mwenyekiti wa Elimu kwa jamii ya Waboni, Bw Eliud Sangu, ambaye pia ni kiongozi wa dini eneo hilo, alisema ukosefu wa elimu miongoni mwa Waboni unasababisha waovu kuendeleza dhuluma hizo bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Bw Sangu alisema licha ya akina baba kujitahidi kuelimisha watoto wao, elimu ya mtoto wa kike eneo hilo haijaona mwangaza kutokana na kwamba akina mama wanaofaa kushinikiza mabinti kuzingatia elimu wamekuwa wakifanya kinyume.
“Kukosekana kwa elimu miongoni mwa jamii kumefanya wakazi wa hapa kukosa kutambua haki zao za kimsingi. Pia hawatambui haki za watoto. Hii ndiyo sababu wazee wanaendeleza uhusiano wa kimapenzi na watoto wa shule waziwazi bila kuogopa,” akaserma Bw Sangu.
Afisa wa Elimu na Haki za Watoto wa Shirika la World Vision eneo la Lamu, Bi Schollar Mghoi alisema tayari wanaendeleza kampeni za kuhamasisha jamii eneo hilo kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Bi Mghoi alisema mimba za mapema zimekuwa kikwazo kwa elimu ya mtoto msichana hasa kwenye tarafa ya Hindi, tangu janga la Covid-19 lilipotangazwa hapa nchini Machi 13, 2020.
“Tumezindua mpango wa kuwaelimisha wasichana na jamii kwa jumla kuhusu umuhimu wa elimu ya mtoto wa kike. Pia tunaihamasisha jamii kuheshimu haki za watoto,” akasema Bi Mghoi.