Gideon Moi akaangwa mazishini kwa 'kukataza' Ruto kusalimia babake
Na FLORAH KOECH
MAGAVANA, maseneta na wabunge Jumamosi walimkabili vikali Seneta wa Baringo Gideon Moi kwa ‘kuhujumu’ azma ya Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022.
Licha ya Bw Ruto na Seneta Moi kusalimiana punde baada ya kuwasili katika mazishi ya mbunge wa Baringo Kusini Grace Kipchoim, eneo la Mochongoi, wandani wa Naibu Rais walimshambulia seneta huyo wakimtaka azime ndoto yake ya kutafuta urais 2022 na kukubali wanasiasa wamtembelee babake, Rais mstaafu Daniel Moi.
Naibu Rais aliwasili kabla ya Seneta Moi na kundi kubwa la wanasiasa kutoka chama cha Jubilee ambao walionekana kuwa tayari kumkabili seneta huyo kwa kumzuia Bw Ruto kukutana na mzee Moi mnamo Ijumaa.
“Wewe ni feki kwa sababu ulimruhusu mtu kutoka nje (ya Rift Valley), Raila Odinga, ambaye alipinga Jubilee katika uchaguzi uliopita kumsalimia babako lakini ukamfungia nje nduguyo,” Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alianza kumrushia Gedion kombora la kwanza. Baadhi ya wanasiasa hao walimuonya Seneta Moi akome kufanya siasa na afya ya babake.
“Wakenya tayari wameamua ni Ruto, iwapo rais mstaafu atasalimiana na watu au la,” alisema mbunge wa Keiyo Kusini, Daniel Rono.
Mbunge wa Marakwet Mashariki Kangogo Bowen aliwaomba wakazi wa Bonde la Ufa kuheshimu viongozi wote wawili.
“Wacheni fahali waendelee kupigana, ikiwa mmoja ataonyesha dalili za kukosa uwezo wa kuzalisha ifikiapo 2022 anafaa kuhasiwa,” alisema Bowen.
Naye mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa alisema Rais Uhuru Kenyatta anaheshimu Katiba, wananchi na naibu wake na kuongeza kuwa Bw Ruto atapeperusha bendera ya Jubilee 2022.
“Usisikilize propaganda iliyoanzishwa na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli,” alisema Bw Ichungwa.
Bw Atwoli alipendekeza kubadilishwa kwa sheria ili kumpa Rais Kenyatta muda zaidi wa kutawala.
Kauli ya Bw Ichungwa iliungwa mkono na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria aliyesema wakati wa siasa za urithi uliisha kitambo nchini.
Mwakilishi wa Kike wa Samburu Maison Leshomo alimtaka seneta huyo kuwaruhusu viongozi wengine kukutana na rais mstaafu Moi.
“Mzee Moi alikuwa rais wetu kwa miaka 24. Sio mali ya mtu yeyote, kama viongozi tunahitaji maarifa katika uongozi,” alisema mbunge huyo wa KANU.
Kauli yake ilisisitizwa na Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet, Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, Mbunge wa Taveta Naomi Shaaban na waziri msaidizi Rachel Shebesh.
Gavana wa Baringo Stanley Kiptis vilevile alimuonya Seneta Moi dhidi ya kugawanya kura za Rift Valley.
‘Msitaje babangu’
Seneta Moi aliyeonekana kukerwa na shutuma dhidi ya familia yake, aliwasihi viongozi wakome kutaja babake katika cheche zao.
“Nawasihi mkome kuhusisha babangu katika suala hili. Sina kinyongo na yeyote anayetaka kujikabili lakini naomba mmutoe babangu katika huu mjadala,”alisema Seneta huyo.
“Kila mtu hapa ni Gideon, Gideon, Gideon…Wakenya wanajua nani wangetaka awaongoze.”
Bw Ruto kwa upande mwingine alihepa suala hilo na badala yake akamsifu marehemu kwa uchapakazi wake hadi wakati wa kifo chake mnamo Aprili 20 kutokana na saratani ya tumbo.
Mnamo Aprili 14, Bw Odinga alimtembelea Mzee Moi nyumbani kwake Kabarak na kupokelewa vyema ambapo Gideon alikuwa miongoni mwa waliomkaribisha.
Mkutano huo ulionekana kama kuidhinishwa kwa muafaka kati ya Raila na Rais Kenyatta na kiongozi huyo wa zamani.