AFUENI: Wachezaji wawili wa raga kusimama kizimbani tena
Na RICHARD MUNGUTI
WACHEZAJI wawili maarufu wa mchezo wa raga waliohukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la ubakaji Jumanne walipata afueni Mahakama Kuu ilipofutilia mbali adhabu hiyo na kuamuru kesi ifanywe upya.
Jaji Grace Ngenye Macharia aliyesikiza rufaa ya Alex Olaba, 24 na Frank Wanyama, 23 aliamuru kesi hiyo isikizwe upya ndipo korti irekebishe kasoro zilizofanywa na upande wa mashtaka.
Sasa Olaba na Wanyana wataachiliwa kutoka gerezani walikokuwa wameanza kutumikia vifungo warudi nyumbani.
Ijapokuwa watafunguliwa mashtaka upya na kiongozi wa mashtaka Everlyne Onungo kuwaita mashahidi upya, wawili hao wataomba korti iwaachilie kwa dhamana wafanye kesi kutoka nje.
Wawili hao walikuwa wamekata rufaa kupinga hukumu dhidi yao wakidai hawakutendewa haki.
Walikuwa wameshtakiwa kumbaka mwanamke mnamo 2018 na walihukumiwa mnamo Agosti 16, 2019, na Bi Mutuku.
Hakimu huyo aliwapata na hatia ya kumbaka mwanamke huyo kwa zamu.
Akinukuu kifungu Nambari 10 ya Sheria za Ubakaji za mwaka wa 2006 hakimu alisema mmoja anayepatikana na hatia chini ya kifungu hiki cha sheria ataadhibiwa kwa kufungwa jela miaka 15.
Akipitisha adhabu, Bi Mutuku alisema ushahidi uliowasilishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Onungo ni kwamba wawili hao walimbaka mwanamke huyo ambaye ni mwanamuziki katika makazi ya Seefar Apartments katika mtaa wa Nyayo Highrise.
Mawakili waliowatetea wafungwa hao walimweleza Jaji Macharia sheria haikufuatwa ipasavyo wakati wa kusikizwa kwa kesi na pia wakati wa kupitisha hukumu.
“Baada ya kusikiza mawasilisho ya wafungwa hawa wawili, nakubaliana nao kwamba sheria haikufuatwa ipasavyo na kesi hii inastahili kusikizwa upya mbele ya hakimu mwingine, sio Bi Mutuku,” aliamuru Jaji Macharia.
Siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo haijatengwa.
Rufaa hiyo ilisikizwa kwa njia ya mtandao wa Zoom.
Wakijitetea kabla ya kuhukumiwa washtakiwa walimweleza hakimu kwamba wao na mlalamishi walikuwa wamelewa chakari na hakuna aliyekuwa anaweza kujidhibiti.
Walijitetea kwamba mlalamishi aliyekuwa na umri wa miaka 24 aliamua kulala katika makazi yao na baadaye akajaribu kudai apewe pesa ndipo awaondolee lawama na kufutilia mbali kesi hiyo ya ubakaji.
Wachezaji hao wa kimataifa wa Raga walikataa kutoa pesa.
Walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Spring Valley.
Akitoa ushahidi kortini mlalamishi alisema yeye ni mwanamuziki na alishawishiwa na washtakiwa kuandamana nao hadi makazi yao.
Alidai wawili hao walimbaka kwa zamu.
Mawakili walieleza mahakama mmoja wachezaji hao alikuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Strathmore na tayari alikuwa amepokea msaada wa masomo kujiunga na chuo kikuu cha Canada ilhali mwenzake alikuwa ametia sahihi kandarasi ya kuchezea klabu.
Wote wawili walikuwa wanachezea timu ya raga ya taifa ya Shujaa.
Olaba na Wanyama walianza kuchezea timu ya Raga ya Chuo Kikuu cha Strathmore maarufu kama Strathmore Leos kabla ya kujiunga na Kenya Harlequins.