• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
Sheffield United wafundisha vijana wa Mourinho kusakata boli

Sheffield United wafundisha vijana wa Mourinho kusakata boli

Na CHRIS ADUNGO

SHEFFIELD United walisajili ushindi wao wa kwanza tangu kurejelewa kwa kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika mchuano uliowashuhudia wakitandika Tottenham Hotspur 3-1 uwanjani Bramall Lane mnamo Julai 2, 2020.

Matokeo hayo yaliweka hai matumaini ya Sheffield United kufuzu kwa soka ya bara Ulaya msimu ujao.

Sheffield almaarufu ‘Blades’ walifungua ukurasa wao wa mabao kupitia kwa Sander Berge ambaye ni sajili ghali zaidi katika historia ya kikosi hicho cha mkufunzi Chris Wilder. Goli hilo lilifumwa wavuni kunako dakika ya 31.

Ingawa fowadi na nahodha Harry Kane alifunga bao dakika chache baadaye, juhudi zake zilifutiliwa mbali na refa kwa madai kwamba alicheka na nyavu za wenyeji wao baada ya kiungo Lucas Moura kuunawa mpira. Maamuzi hayo yalithibitishwa baada ya kurejelewa kwa teknolojia ya VAR.

Ingawa Tottenham walitarajiwa kukizamisha chombo cha Sheffield United kirahisi, masogora hao wa kocha Jose Mourinho walisuasua pakubwa huku wakionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara.

Badala yake, ni vijana wa Wilder ndio waliopachika wavuni bao la pili kupitia kwa Lys Mousset katika dakika ya 69 baada ya kukamilisha krosi ya Enda Stevens kwa ustadi mkubwa.

Bao la tatu la Sheffield lilifumwa wavuni kupitia kwa Oli McBurnie ambaye kwa sasa anajivunia mabao matano ya EPL msimu huu.

Kane ambaye alishuhudia bao lake jingine likifutiliwa mbali kwa kuotea wakati matokeo yalipokuwa 2-0, alicheka na nyavu za wenyeji wao hatimaye mwishoni mwa kipindi cha pili na kufanya mambo kuwa 3-1.

Goli hilo lilikuwa zao la Kane ambaye kwa sasa ana jumla ya magoli 13 kibindoni, kushirikiana vilivyo na mshambuliaji mwenzake, Son Heung-min.

Ushindi kwa Sheffield United uliwapaisha hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 47, saba pekee nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora kileleni. Ni pengo la pointi tano ndilo linatamalaki kati ya Sheffield na Manchester United na Wolves wanaokamata nafasi za tano na sita mtawalia.

Tottenham ambao hawajawahi kukamalisha kampeni za EPL nje ya orodha ya sita-bora tangu 2009, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa kwa alama saba zaidi nyuma ya Wolves ambao wamejizolea pointi 52.

Sheffield walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo dhidi ya Tottenham wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kufungwa jumla ya mabao sita kutokana na mechi mbili za awali.

Baada ya kuvaana na Burnley mnamo Julai 5, Sheffield wamepangiwa kupepetana na Wolves, Chelsea, Leicester City na Everton kwa usanjari huo. Kwa upande wao, Tottenham watamenyana na Everton, Bournemouth na Arsenal kabla ya kukwaruzana na Newcastle, Leicester ba Crystal Palace mtawalia.

You can share this post!

Mabingwa Liverpool wapokezwa kichapo cha 4-0 uwanjani Etihad

Sergio Ramos afunga penalti kusaidia Real Madrid kufungua...

adminleo