Waathiriwa wa mafuriko Afrika Mashariki wakodolea macho njaa
Na CHRIS OYIER
Kwa muhtasari:
- Nchi za Afrika Mashariki zimekumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha eneo hilo
- Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya takriban wati 120 nchini Kenya, watu 116 nchini Rwanda, 14 nchini Tanzania na watu 3 nchini Uganda
- Mafuriko hayo yaliyoshuhudiwa yamewaacha maelfu ya raia bila makazi na chakula
- Huenda tukio hilo likasababisha njaa katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo
TOFAUTI na ukame ulioshuhudiwa mwanzoni mwa mwaka wa 2017 katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, mwaka wa 2018 umekuwa tofauti kwani mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha yasababisha mauti, kuharibu nyumba na mali huku kilimo kikipata pigo.
Hali hiyo imeshuhudiwa katika nchi zote za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya ambapo kulingana na shirika la Msalaba Mwekundu, takriban watu 120 wamefariki na maelfu wengine kuachwa bila makao katika kaunti 32 zilizoathirika zaidi na mafuriko.
“Familia 48, 177 zimeachwa bila makao, hali ambayo inawaacha jumla ya watu 260,200 bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji,” Katibu Mkuu wa shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya Abbas Gullet alisema.
Nchini Tanzania, hali ni mbaya kwani watu 14 wameripotiwa kufariki huku Uganda ikiandikisha vifo vya watu 3.
Kulingana na jarida la Uganda la New Vision, wanajeshi wa AMISOM nchini Somalia waliwaokoa takriban watu 10,000 kutoka eneo la Beledwenye, kusini mwa nchi hiyo ambayo nyumba, mifugo na mimea ilisombwa na maji.
Nchini Rwanda watu 116 waliripotiwa kufariki kutokana na mafuriko huku mamia ya watu wengine wakiachwa bila makao.
Waathiriwa wa mafuriko wanaishi kwa hofu ya kutegemea msaada baada ya mimea yao kusombwa na maji katika nchi hizo.
Ijumaa, Mei 4, shirika la Msalaba Mwekundu liliwaomba Wakenya kuisaidia kuchangisha Sh500 milioni ili kushughulikia mahitaji ya waathiriwa wa mafuriko ambao wanahitaji vyakula, malazi, dawa na vifaa vya kutumia.
Hata hivyo, shirika hilo lilikiri kuwa kukabiliana na athari za mafuriko kutachukua muda, ikizingatiwa kuwa linategemea msaada kuwapa waathiriwa hao chakula.
Mwezi Machi, serikali ya kaunti ya Nairobi ilitenga KSh 194 milioni kurekebisha miundo msingi ili kuzuia mafuriko katika sehemu kadhaa za jiji.
Serikali kuu nchini Kenya haijatangaza itakavyowasaidia waathiriwa na mafuriko ambao wako kwenye hatari ya kukosa chakula kutokana na mimea yao kusombwa na maji na ikizingatiwa hawawezi kurejea katika mashamba yao yaliyofurika kwa sasa kuendeleza kilimo.