Kimataifa

Watu 160 wauawa kwenye maandamano Ethiopia

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

WATU 160 wameuawa nchini Ethiopia kufuatia maandamano makali ambayo yamelikumba taifa hilo kwa siku kadhaa kutokana na mauaji ya mwanamuziki maarufu, Hachalu Hundessa, polisi wamesema.

“Kutokana na hali ambayo ilitokea baada ya kifo cha Hacaaluu, raia 145 na maafisa 11 wa usalama wamepoteza maisha yao kwenye maandamano hayo,” akasema Girma Gelam, ambaye ndiye Naibu Kamishna wa Polisi katika eneo la Oromia.

Alisema hayo Jumamosi kwenye mahojiano na kituo cha habari cha serikali, Fana Broadcasting Corporation.

Watu wengine 10 waliripotiwa kufariki jijini Addis Ababa.

Kamishna huyo alisema kuwa watu wengine 167 walipata majeraha mabaya huku 1,084 wakikamatwa.

Mwanamuziki huyo, ambaye anatoka katika jamii ya Oromo, alipigwa risasi na watu ambao hawajulikani Jumatatu iliyopita jijini Addis Ababa. Ni hali ambayo imezua taharuki kubwa za kikabila na kisiasa, ambazo zimetishia kusambaratisha uthabiti wa kidemokrasia nchini humo.

Jamii ya Oromo ndiyo kubwa zaidi katika taifa hilo.

Kulingana na polisi, watu watano wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Na licha ya hayo, vikosi vya usalama vimekuwa vikidai kwamba huenda kundi la wapiganaji la Oromo Liberation Front (OLF) na chama cha upinzani cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF) ndivyo vilihusika.

Maafisa wa serikali wamesema kuwa vifo hivyo vilisababishwa na masuala kadhaa, baadhi yakiwa hali ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na ghasia za kikabila.

Hata hivyo, mkuu huyo wa polisi alisema kuwa ghasia hizo sasa zimeisha kabisa.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Abiy Ahmed alisema kuwa mauaji ya mwanamuziki huyo ni njama inayoendeshwa kichinichini na baadhi ya watu “kuvuruga uthabiti wa taifa hilo.”

Miongoni mwa watu ambao wamekamatwa kufikia sasa ni viongozi watatu wakuu wa upinzani, akiwemo Jawar Mohammed. Mohammed alikuwa mmiliki wa vyombo kadhaa vya habari vyenye ushawishi.

Licha ya kukamatwa kwao, hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu kesi zinazowakabili.

Haaacaaluu, 36, alizikwa mnamo Alhamisi chini ya usimamizi mkali wa polisi na jeshi katika mji wa Ambo, anakotoka. Alimwacha mjane na watoto wawili.

Nyimbo za mwanamuziki huyo zilikuwa zikitetea maslahi ya jamii ya Oromo, hasa dhidi ya ubaguzi na dhuluma za kisiasa kabla ya Abiy kuchukua uongozi mnamo 2018.