Changamoto kuzuia wazee katika ibada
Na BENSON MATHEKA
UAMUZI wa serikali kwamba wazee wa zaidi ya umri wa miaka 58 wasikubaliwe kuingia katika maeneo ya ibada umeacha viongozi wa dini mataani.
Katika madhehebu mengi nchini, wahubiri na wasimamizi wakuu wa maeneo ya ibada huwa ni wa umri mkubwa. Hitaji hilo lilitangazwa Jumatatu, wakati Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza kanuni mpya kuhusu kudhibiti virusi vya corona, ambapo pia watoto wa chini ya miaka 13 hawatakubaliwa kuingia maeneo ya ibada.
Jana, Baraza la Mashirika ya Kidini lilisema maeneo ya ibada yataanza kufunguliwa Jumanne ijayo lakini kila dhehebu litajiamulia kuhusu viongozi wa dini waliopita miaka 58.
Wataalamu wa afya husema wazee na wagonjwa wamo hatarini zaidi kuathirika sana na virusi vya corona.
“Viongozi wa maeneo hayo watakuwa na jukumu la kuhakikisha mwongozo wa kuzuia maambukizi ya corona utazingatiwa kikamilifu,” alisema mwenyekiti wa baraza hilo Askofu Mkuu wa dayosisi ya Nyeri ya kanisa Katoliki Antony Muheria.
Iliamuliwa kuwa ibada zitakuwa zikichukua saa moja pekee na kuhudhuriwa na watu wasiozidi 100 kwa wakati mmoja.
Ili kuhakikisha masharti ya kuzuia kusambaa kwa corona yatazingatiwa, kutakuwa na kamati ya viongozi wa dini mbali mbali katika kila kaunti ndogo na pia katika kiwango cha kaunti.
Kila eneo la kuabudu litakuwa na kamati ya kukabiliana na corona.
“Litakuwa jukumu la viongozi wa kidini kuhakikisha kuwa mwongozo wa kufungua eneo lao la ibada na kanuni za wizara ya afya na Shrika la Afya Ulimwenguni (WHO) zitazingatiwa,” alisisitiza Askofu Muheria.
Aliwahimiza viongozi wa kidini kutoharakisha kufungua maeneo yao ya kuabudu kabla ya kuweka mipango inayofaa.
Kulingana na mwongozo uliotolewa na baraza hilo, maeneo ya kuabudu ni sharti yawe na maji ya waumini kuosha mikono au sanitaiza, waumini kuketi umbali wa mita moja na nusu kutoka kila mmoja, kuosha maeneo hayo mara kwa mara.
Waumini wote watakuwa wakipimwa viwango vya joto kabla ya kuruhusiwa kuingia makanisani na misikitini na kila mmoja lazima avalie barakoa.
Askofu Muheria aliwataka Wakenya kutumia kufunguliwa kwa maeneo ya kuabudu kuombea nchi na ulimwengu wakati huu wa janga la corona.