Habari MsetoSiasa

Maseneta wachemka wakipinga mfumo mpya wa ugavi wa fedha

July 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

NA CHARLES WASONGA

ZAIDI ya maseneta 21 wamepinga mfumo mpya wa ugavi wa fedha baina ya kaunti uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) na wakaapa kutoupitisha katika Seneti.

Maseneta hao kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki, Mashariki, Pwani na Nyanza walisema mfumo huo unaozipa uzito mkubwa vigezo kama vile huduma za kilimo na afya utachangia maeneo yao kupokonywwa fedha nyingi.

Fedha hizo, wanasema, zitaelekezwa katika kaunti ambazo zina utajiri mkubwa katika nyanja ya kilimo kando na kuwa na idadi kubwa ya watu.

Viongozi hao walisema mfumo huo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti utazinyima fedha za maendeleo kaunti ambazo zimesalia nyuma kimaendeleo tangu enzi ya ukoloni.

Miongoni mwa maseneta waliopinga mfumo huo wa ugavi wa fedha ni; Ledama Ole Kina (Narok), Steward Madzayo (Kilifi), Mohamed Faki (Mombasa), Sam Ongeri (Kisii), Enoch Wambua (Kitui), Boy Juma (Kwale), Johannes Mwaruma (Taita Taveta), Okongo Omogeni (Nyamira), Fatuma Dullo (Isiolo), Malik Ekal (Turkana).

Wengine walikuwa Yusuf Haji (Garissa), Mohammed Mahamud (Mandera), Abdirahman Ali Hassan, Abishiro Halake (Seneta Maalum), miongoni mwa wengine.

Wakiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, Jumanne, maseneta hao walisema mfumo huo mpya utaathiri pakubwa wakazi wa maeneo kame nchini.

“Huu mfumo uliopendekezwa na Mithika Linturi (Seneta wa Meru) utachangia jumla ya kaunti 18 nchini kupoteza jumla ya Sh17 bilioni ikiwa utaidhinishwa na Seneti na kutumika katika mwaka wa kifedha ulioanza Julai mosi,” akasema Seneta Mahamud ambaye juzi alipokonywa wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Fedha.

“Na inaudhi kuwa sasa suala hili nyeti linajadiliwa nje ya seneti baada ya mkutano wa Kamukunji ulioitishwa na Spika kuwekwa kando,” akaongeza.

Naye Bw Wambua (Kitui) alisema mfumo wowote wa ugavi wa fedha kwa kaunti sharti uhakikishe kuwa hakuna kaunti inayopoteza fedha zozote ikilinganishwa na hali ilivyokuwa chini ya mfumo wa awali.

“Ugatuzi hauwezi kufaulu ikiwa kaunti ambazo zimebaki nyuma kimaendeleo zitapokonywa fedha na kupewa kaunti ambazo zimefaidi kimaendeleo tangu enzi ya ukoloni. Kwa mfano, chini ya mfumo huu, mpya kaunti yangu ya Kitui itapoteza kima cha Sh800 milioni. Siwezi kuunga mkono mfumo kama huu ilhali nilichaguliwa kutetea watu wangu,” akasema Bw Wambua.

Naye Seneta wa Wajir Bw Abdirahman Ali akasema: “Iweje kaunti yangu ipokinywe Sh2 bilioni huku kaunti ya Kiambu ikiongezwa Sh1.5 bilioni? Mbona wale ambao wako na utajiri mwingi ndio wanaongezewa?”

Kiongozi huyo alisema wale waliobuni mfumo huo wanaendeleza njama ya kutwaa matunda ya ugatuzi ambayo kaunti za maeneo kame zilikuwa zimeanza kuvuna.

“Hatutaruhusu kaunti zetu kutengwa kimaendeleo kwa mara nyingine,” akasema Seneta Ali.

Naye Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo alipendekeza kuwa mfumo wa zamani wa ugavi wa fedha baina ya kaunti utumiwe mwaka huu huku maelewano kuhusu mfumo huu mpya yakitafutwa.

“Kaunti yangu ya Isiolo itapoteza Sh869 milioni na bajeti yetu ni Sh4.9 bilioni. Hii ina maana kuwa huenda tukafikia wakati ambapo tutalazimika kufunga kaunti ya Isiolo,” akasema Seneta huyo ambaye ni Naibu Kiongozi wa Wengi katika Seneti.

“Ikiwa tutaanza kuzinyima kaunti zingine fedha na kuziongezea zingine. Sasa tutakuwa tunapalilia ugatuzi ama tunaua kabisa?” akauliza Bi Dullo.

Kwa upande wake Seneta wa Garissa Mzee Yusuf Haji alisema: “Hakuna popote palipoandikwa katika Bibilia au Quran kwa unapasa kumpokonya mtu mmoja ili umpe mwingine. Sisi ni wanadamu na hatuwezi kuruhusu vichwa vyetu vikatwe. Pesa zetu zikitwaliwa, ina maana kuwa hakuna ugatuzi.”

Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo naye alisema chini ya mfumo huo mpya kaunti zote sita za Pwani mwa Kenya zitapoteza jumla ya Sh7 bilioni.

“Hii sio haki. Pesa haziwezi kutolewa kwa masikini na kupelekwa kwa matajiri,” akasema.

Kwa upande wake Seneta wa Kisii Profesa Sam Ongeri alisema yeye na mwenzake wa Nyamira Okong’o Omogeni watapinga mfumo huo kwa kuwa kaunti zao zitapoteza jumla ya Sh800 milioni.

“Hii sio haki kwa sababu kaunti zetu zina idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma na miradi ya maendeleo sawa na wananchi kutoka maeneo mengine,” akasema Seneta huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC).

Seneta Malik Ekal wa Turkana alisema sio haki kwamba kaunti yake itapokonywa fedha ilhali imebaki nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi.

“Wakazi wa Turkana ni Wakenya na wanahitaji barabara na miradi ya maji kama watu kutoka sehemu zingine,” akasema Profesa Ekal.

Bw Ole Kina wa Narok alidai kuwa wale wanaounga mkono mfumo huo wana nia mbaya ya kulemaza maendeleo katika maeneo ya wafugaji, Waislamu na jamii zingine ndogo ndogo za humu nchini.

“Hatuwe kukubali njama hii ya kuigawanya Kenya kuwili. Sisi sote ni Wakenya na tunafaa kutendewa haki na usawa,” akasema.