Habari Mseto

Magoha ashauri wazazi warudishiwe karo

July 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, ameshauri wasimamizi wa shule kurudishia wazazi karo endapo walikuwa wamelipia muhula wa pili na watatu.

Akizungumza na wanahabari jana, Prof Magoha alisema ni karo ya muhula wa kwanza pekee ambayo ilitumiwa kwani watoto walikuwa shuleni kwa miezi kadhaa.

Kwa upande mwingine, alisema hakuna masomo yamefanyika shule za msingi na upili muhula wa pili, na hakutakuwa na masomo muhula wa tatu kufuatia agizo la kufutilia mbali kalenda ya masomo mwaka huu.

‘Karo ya muhula wa kwanza ilitumiwa. Muhula wa pili haijakuwa kwa hivyo aliyelipa anafaa arudishiwe,’ akasema.

Hata hivyo, alitambua kuwa huenda kukawa na maelewano kati ya baadhi ya shule, hasa za kibinafsi, na wazazi kuhusu ulipaji wa karo.

Kuna shule za kibinafsi ambazo zingali zinaendelea kutoa mafunzo kwa njia ya mitandao na wazazi wanahitajika kugharamia malipo ya walimu husika na rasilimali nyingine ambazo zinatumika.

‘Kama walimu watashawishi wazazi jinsi hizo pesa zinatumiwa, ni sawa. Lakini kila mtu anatarajia arudishiwe karo au zihamishwe hadi mwaka ujao,’ akasema.