ODM yajiandaa kupinga refarenda kufanywa 2022
Na SAMWEL OWINO
CHAMA cha ODM kimepanga mikakati kuzuia uwezekano wa bunge kupitisha hoja ambayo itapelekea kura ya maamuzi kufanywa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka wa 2022.
Chama hicho kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, kinapendelea kura ya maamuzi kufanywa siku 90 baada ya hoja kuhusu refarenda kupitishwa.
Kufikia sasa, kuna hoja mbili zinazoshughulikiwa wakati ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) inaposubiriwa.Moja imependekezwa na Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC), inayotaka kura ya maamuzi ifanywe 2022, na nyingine inapendekezwa na Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) ambayo ndiyo inaungwa mkono na ODM.
Imefichuka Bw Odinga aliagiza mawakili na wataalamu wake wa kisheria kukagua hoja zote mbili, ikaamuliwa ile ya JLAC ndiyo nzuri.
Kwa upande mwingine, chama hicho kimetilia shaka hoja ya CIOC ambayo inapigiwa debe na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Jeremiah Kioni, viongozi wakionekana kushuku imefadhiliwa na Naibu Rais William Ruto.
Viongozi wa ODM wamesema mkakati wao wa kwanza utakuwa kumshawishi Bw Kioni aachane na mipango yake.
‘Endapo tutakubaliana kwamba mswada wa JLAC ndio utaletea nchi katiba bora, basi atahitajika kuondoa ile yake. Hiyo ndiyo njia rahisi zaidi,’ mwanachama wa JLAC aliyeomba asitajwe gazetini akasema.
Mpango wa pili utakuwa ni kumshawishi Spika wa Bunge la Taifa, Bw Justin Muturi kutumia mamlaka yake ili aamue kwamba bunge haliwezi kufuatilia miswada miwili katika kamati tofauti ilhali ni miswada inayohusu jambo moja linalofanana.
Endapo mikakati hiyo miwili itagonga mwamba, miswada yote itaruhusiwa kuendelezwa mbele lakini wabunge watashawishiwa kutilia maanani ule wa JLAC hadi uidhinishwe na Rais Uhuru Kenyatta.
Kiongozi wa wachache bungeni, Bw John Mbadi, jana alithibitisha kuwa ODM iliamua mswada wa Bw Kioni unashukiwa kufadhiliwa na watu wanaopinga kura ya maamuzi.
‘Sijui nani aliufadhili, lakini tunaushuku na pia haijulikani wazi jinsi mswada huo ulivyofika bungeni,’ akasema Bw Mbadi.
Mwenyekiti huyo wa ODM alisema Kamati ya Shughuli za Bungeni (HBC) ambayo huamua ajenda za bunge ilikutana na kuamua kuunganisha miswada hiyo miwili ili kuwe na moja pekee.
Chama hicho kinategemea ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, pamoja na jinsi wandani wa Dkt Ruto walivyotimuliwa kutoka kwa kamati muhimu, zitasaidia kufanikisha mipango ya kufanyia katiba mabadiliko jinsi wanavyopendekeza.
Naibu Katibu wa Chama cha Jubilee, Bw Caleb Kositany ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, alisema itakuwa makosa kuondoa mswada wa CIOC kwa msingi wa pendekezo lake la kutaka kura ya maamuzi ifanywe pamoja na Uchaguzi Mkuu.
Alipuuzilia mbali pia wanasiasa wanaomhusisha Dkt Ruto na mswada huo wa Bw Kioni.’Inafaa watu waendelee mbele na maisha yao, wakome kumtaja Naibu Rais kila mara bila sababu.
Naibu Rais ana shughuli nyingine muhimu za kufanya,’ akasema.