• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Wanaovumisha Ruto 2022 wakome – Fred Ouda

Wanaovumisha Ruto 2022 wakome – Fred Ouda

Na LUCY KILALO

MBUNGE wa Kisumu ya Kati, Fred Ouda amewataka baadhi ya viongozi wa Rift Valley wanaompigia debe Naibu Rais William Ruto wawache kubabaika kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa 2022, akisema kuna wengi wanaoweza pia kuwania.

Mbunge huyo pia aliwaonya dhidi ya kumpa Rais Uhuru Kenyatta masharti kuhusiana na uchaguzi huo.

Akihutubia wanahabari Jumatano katika majengo ya Bunge, Bw Ouda alimshtumu hasa Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen kwa kuonekana kusisitiza kuwa Naibu Rais William Ruto ndiye atawania urais 2022.

“Kwa sasa Rais Kenyatta ana ajenda moja, ambayo ni kuacha sifa njema, na lazima aungwe mkono,” alisema.

Mbunge huyo pia aliwasuta viongozi hao akisema wanastahili kutambua kuwa sio Bw Ruto pekee anaweza kuwania urais nchini.

“Wengi nchini wanaweza kuwania urais na sio kwa vitisho. Pia kinachoamua ni tabia yako, marafiki na kile umefanyia nchi na sio kupendekezwa.”

Aliongeza, “Rift Valley ina watu wengine, ingawaje kufikia sasa ni Seneta wa Baringo Gideon Moi na Bw Ruto ambao wameonyesha nia. Hata hivyo, Bw Moi ana haki ya kuwania na ninamhimiza awanie. Wacha awashawishi Wakenya sawa na Bw Ruto.”

Juma lililopita katika mazishi ya mbunge wa Baringo Kati, Bi Grace Kipchoim, viongozi hao walimtaka Bw Moi kutelekeza azma yake ya kuwania urais.

Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa pia alionya ushindani wa kisiasa dhidi ya viongozi hao kutoka jamii ya Kalenjin kuwa huenda ukawanyima urais 2022 na pia kumtaka Bw Moi kutowania.

Alisema kuwa Jubilee ilifanya mkataba ambapo rais Kenyatta alikuwa aongoze kwa kipindi cha mwisho, na kisha eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono Bw Ruto 2022.

 

 

You can share this post!

Tahadhari kuhusu Ebola

Mwanahabari abubujikwa na machozi baada ya kuponea...

adminleo