Habari MsetoSiasa

2022: Ford-Kenya yamkemea Eugene

August 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha Ford Kenya kimemkemea waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa kwa kusema kuwa atahakikisha kitashirikiana na chama cha Kanu kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Wamalwa alisema hayo alipoongoza ujumbe wa viongozi wa eneo la Magharibi mwa Kenya kumtembelea Mwenyekiti wa Kanu Gedion Moi nyumbani kwake Kabarak mnamo Jumamosi.

Jana, Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa alisema Bw Wamalwa sio mwanachama wa Ford Kenya na hivyo hawezi kuzungumza kwa niaba ya chama hicho.

‘Kama chama, tunataka kujitenga naye na kufafanua kuwa hana mamlaka ya kisheria au vingine kuwakilisha chama cha Ford Kenya au kuzungumza kwa niaba yake,” alisema Bw Wamalwa anayeegemea upande wa Seneta wa Kaunti ya Bungoma, Moses Wetangula kwenye mzozo wa uongozi wa chama hicho.

Bw Wetang’ula alimteua Bw Wamalwa kaimu katibu mkuu baada ya Dkt Eseli Simiyu kuongoza mapinduzi ya kumvua wadhifa wa kiongozi wa chama hicho. Kwenye taarifa yake, Bw Wamalwa alisema Ford Kenya kina mifumo ya kisheria ya kuunda miungano ya kisiasa na hakihitaji mabroka wa kisiasa.

“Imenakiliwa kwamba Wamalwa aliuzia Jubilee chama chake cha New Ford Kenya na kama anataka kujiunga na siasa kikamilifu, tunamwambia ajiuzulu rasmi wadhifa wake kujiunga na siasa kikamilifu,” alisema Bw Wamalwa.

Katika ziara yake Kabarak, Waziri Wamalwa alikuwa ameandamana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyikazi (Cotu) Francis Atwoli, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Emmanuel Wangwe miongoni mwa viongozi wengine.

Waziri Wamalwa, Oparanya na Bw Atwoli wamekuwa wakiongoza kampeni ya kupigia debe mpango wa BBI eneo la Magharibi ambayo imesusiwa na Bw Wetangula na kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.