• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Ni wakati wetu kupata maendeleo, wafoka wabunge wa maeneo kame

Ni wakati wetu kupata maendeleo, wafoka wabunge wa maeneo kame

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE kutoka maeneo kame nchini (ASAL) wamewataka maseneta kutupilia mbali mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti mjadala kuhusu suala hilo utakaporejelewa Jumanne wiki hii.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Kundi la Wabunge kutoka Jami za Wafugaji (PPG) Alois Lentoimaga wabunge hao walidai maseneta wanaounga mkono mfumo wa ugavi unaoongeza fedha kwa kaunti 18 zenye idadi kubwa ya watu wanalenga kuligawanya taifa hili kuwili.

“Watu kutoka jamii zilizobaki nyuma kimaendeleo pia wana haki ya kupata maendeleo. Kaunti zao hazifai kupokonywa fedha ili kaunti zilizoendelea ziongezewe,” akasema mbunge huyo wa Samburu Kaskazini..

Naye naibu mwenyekiti wa muungano huo Bashir Abdullahi Sheikh (Mandera Kaskazini) akasema: “Ieleweke kuwa tunauliza haki yetu, wala hatuombi kusaidiwa kwa njia yoyote. Tunaitisha kile ambacho ni haki yetu. Tuko hapa leo kushinikiza kuwa haki na usawa zizingatiwe wakati wa ugavi wa mapato”

Wabunge hao saba walisema demokrasia inahitaji kwamba rasilimali isambazwe kwa njia sawa katika pembe zote za nchini, kwa sababu “Kenya ni taifa moja.”

“Kwa hivyo, mfumo ambao unapasa kuzingatiwa ni ule unaoweka Kenya pamoja. Hatutaki mfumo utakaopelekea watu wetu kuhisi kuwa wametengwa,” Bw Bashir akawaambia wanahabari katika mkahawa wa Sagret, Nairobi.

Wengine waliokuwepo ni Mbunge Mwakilishi wa Isiolo Rehema Jaldesa, Ali Wario Guyo (Garsen), Qalicha Gufu Wario (Moyale) na Sophia Abdinoor (Ijara).

Walisisitiza kuwa ugavi wa fedha unapasa kuzingatia mahitaji ya maendeleo katika kaunti husika.

“Wale wanaounga mkono mfumo huu sharti wafahamu kuwa ukosefu wa maendeleo katika maeneo kame nchini ni zao la sera mbaya zilizobuniwa na baba na mababu zao,” akasema Bw Lentoimaga.

“Tunawataka kesho (Jumanne) maseneta waongozwe na ukweli kwamba kiwango cha umasikini ni juu zaidi katika kaunti za kaskazini mwa Kenya kuliko zile za maeneo ya Kati mwa Kenya na Rift Valley ambazo zitafaidi kutokana na mfumo unaopendekezwa,” akaongeza.

.Wabunge hao walisema kuwa maseneta wanaounga mkono mfumo uliopendekezwa katika ripoti ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na kauli mbiu ya mtu moja shilingi moja wanahujumu Katiba inayohiomiza usawa katika usimamizi wa kifedha.

You can share this post!

Siasa za ugavi wa pesa zachangia kufifia kwa umaarufu wa...

Hakuna ulegevu ndani ya ODM – Mbadi

adminleo